×

Waziri wa Fedha Amkaribisha Rais Samia Kigali Kushiriki Mkutano wa NEISA 2026

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,  Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwasili katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Kigali ambapo atashiriki Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali kuhusu Uvumbuzi wa Nishati ya Nyuklia barani Afrika (NEISA), Kigali nchini Rwanda tarehe 19 Mei, 2026. Mkutano huo wa Kimataifa unawakutanisha pia wataalamu wa nishati, wawekezaji na mashirika ya kimataifa, ambapo utajadili matumizi ya nishati ya nyuklia kwa maendeleo ya Bara la Afrika. Mkutano huo pia unalenga kujadili namna bora ya kuongeza upatikanaji wa nishati ya umeme Afrika, kupunguza uchafuzi wa mazingira, kusaidia maendeleo ya viwanda, kukuza ubunifu wa teknolojia za nishati ya nyuklia pamoja na kuvutia wawekezaji katika miradi ya nishati.

Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), ameshiriki mapokezi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan aliyewasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kigali nchini Rwanda, ambapo anatarajiwa kushiriki Mkutano wa Pili wa Uvumbuzi wa Nishati ya Nyuklia barani Afrika (NEISA 2026).

Mkutano huo wa NEISA unawakutanisha Viongozi wa Serikali, wataalam wa sekta ya nishati, wawekezaji na wadau mbalimbali kutoka mataifa ya Afrika na duniani kwa lengo la kujadili nafasi ya nishati ya nyuklia katika kuimarisha usalama wa nishati, viwanda na maendeleo endelevu barani Afrika.

Mkutano huo wa NEISA 2026 unatoa nafasi kwa Tanzania kushiriki katika ajenda ya Afrika ya matumizi salama ya teknolojia ya nyuklia katika nishati, afya, kilimo, viwanda na utafiti.

Leave a Comment