
Meli mbili kubwa za China zilizobeba mafuta zimeonekana zikitoka katika Mlango wa Hormuz, hatua ambayo imeongeza matumaini ya kupungua kwa mzozo kati ya Marekani, Israel na Iran, kufuatia ishara za mazungumzo ya kidiplomasia yanayoendelea.
Taarifa za ufuatiliaji wa meli zinaonyesha kuwa meli hizo zilipita salama katika eneo hilo nyeti la usafirishaji wa mafuta duniani, hali iliyosaidia kupunguza wasiwasi wa usumbufu mkubwa wa usambazaji wa nishati duniani.
Rais wa Marekani Donald Trump amesema mzozo huo unaweza kumalizika haraka sana, huku Makamu wa Rais JD Vance akieleza kuwa mazungumzo na Tehran yanaendelea vizuri kuelekea makubaliano ya kumaliza uhasama.
“Kwa sasa tupo katika hatua nzuri,” alisema Vance katika mkutano na waandishi wa habari Ikulu ya Marekani.
Trump pia alieleza kuwa alikuwa karibu kuidhinisha mashambulizi mapya dhidi ya Iran, lakini akasimamisha uamuzi huo kufuatia pendekezo jipya la mazungumzo kutoka Tehran.
Hata hivyo, mazungumzo hayo bado yana changamoto kutokana na tofauti za msimamo kati ya pande zinazohusika, huku Marekani ikisisitiza “mipaka yake” katika makubaliano yoyote.
Wakati huo huo, Iran imewasilisha mapendekezo yanayojumuisha kusitishwa kwa uhasama, kuondolewa kwa vikwazo, na kurejeshwa kwa mali zilizozuiwa nje ya nchi, lakini Marekani imeyataja baadhi ya masharti hayo kuwa hayakubaliki.
Mgogoro huo umeathiri kwa kiasi kikubwa sekta ya nishati duniani, ukisababisha kupanda kwa bei ya mafuta na kusababisha mamilioni ya mapipa kushindwa kusafirishwa kwa wakati kupitia Mlango wa Hormuz,.