
Rais wa China, Xi Jinping amemkaribisha Rais wa Urusi, Vladimir Putin Beijing katika mkutano maalum uliolenga kuimarisha uhusiano wa nchi hizo mbili, huku ukitafsiriwa kama ujumbe wa kisiasa kwa dunia kuhusu mshikamano wao wa kimkakati.
Mkutano huo umefanyika siku chache baada ya ziara ya Rais wa Marekani, Donald Trump nchini China, hali iliyotafsiriwa na wachambuzi kama hatua inayoonesha ushindani wa ushawishi kati ya mataifa makubwa duniani.
Putin alipokelewa kwa sherehe rasmi katika Jumba Kuu la Umma la Beijing, ambapo baadaye viongozi hao wawili walifanya mazungumzo ya faragha na pia walitarajiwa kusaini mikataba ya ushirikiano katika sekta mbalimbali.
Ajenda kuu za mazungumzo hayo ni pamoja na nishati, usalama na kuimarisha uhusiano wa kibiashara kati ya China na Urusi, huku mataifa hayo yakiendelea kushirikiana kwa karibu tangu kuanza kwa mzozo wa Ukraine mwaka 2022.
China imeendelea kuwa mshirika mkubwa wa kibiashara wa Urusi, hasa katika ununuzi wa mafuta na gesi, licha ya vikwazo kutoka mataifa ya Magharibi.
Putin amesisitiza kuwa uhusiano kati ya Moscow na Beijing ni muhimu kwa utulivu wa kimataifa, huku akieleza kuwa ushirikiano wao unasaidia kuleta usawa wa nguvu duniani.
Mkutano huo unaonekana kuimarisha zaidi ushirikiano wa kimkakati kati ya China na Urusi katika mazingira ya ushindani mkali wa kidiplomasia duniani.