×

Wafanyabiashara Dodoma Wapewa Mafunzo Ya Ujasiriamali Na Nishati Safi

Dodoma, Tanzania, Jumanne 19 Mei 2026: Stanbic Bank Tanzania, kupitia Stanbic Biashara Incubator, kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo la Ujerumani (GIZ), na Said Salim Bakhresa (SSB) imeendeleza dhamira yake ya kuwawezesha wanawake na vijana wajasiriamali kwa kufikisha programu ya RISE Mama Lishe mkoani Dodoma, ambapo wajasiriamali 320 wa biashara za chakula wanapatiwa mafunzo ya vitendo pamoja na majiko banifu yatakayowasaidia kupunguza gharama, kuboresha usalama na kuimarisha biashara zao.

Tukio la Dodoma ni mwendelezo wa programu ya kitaifa iliyozinduliwa Dar es Salaam mwezi Novemba 2025. Tangu kuzinduliwa kwake, programu hii imeendelea kufika katika mikoa mbalimbali ikiwemo Dar es Salaam, Arusha, Kilimanjaro na Tanga, huku Dodoma ikiwa ni sehemu muhimu katika kupanua wigo wa mpango huu kwa wajasiriamali waliopo katika makao makuu ya nchi.

Kupitia awamu ya mwaka 2025 hadi 2026, Stanbic Bank na GIZ wanalenga kuwawezesha wanawake na vijana wajasiriamali wapatao 2,000 kwa kuwapatia elimu ya biashara, stadi za usimamizi wa fedha, uelewa wa matumizi ya nishati safi ya kupikia na vifaa vinavyogusa mahitaji halisi ya biashara zao za kila siku. Kwa Dodoma, wajasiriamali 300 watakaoshiriki programu hii watapatiwa kila mmoja jiko banifu kama sehemu ya jitihada za kuhamasisha matumizi ya nishati safi na salama ya kupikia.

Kwa Mama na Baba Lishe wengi, jiko salama si kifaa cha kupikia pekee. Ni nyenzo ya kupunguza gharama za nishati, kupunguza madhara ya moshi, kuboresha mazingira ya kazi na kuwapa nafasi zaidi ya kuzingatia wateja, ubora wa huduma na ukuaji wa biashara zao. Kipengele cha nishati safi ya kupikia kinaunga mkono pia lengo la Taifa la kufikia matumizi makubwa ya nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2032, kwa kuhamasisha matumizi ya teknolojia bora za kupikia na kupunguza utegemezi wa kuni na mkaa.

Programu ya RISE Mama Lishe inaendeleza uwekezaji mpana wa Stanbic Bank katika ukuaji wa biashara ndogo na za kati. Katika kipindi cha miaka minne iliyopita, benki imewawezesha zaidi ya wajasiriamali 3,000 kupitia mafunzo, ushauri, elimu ya fedha na msaada wa vitendo unaolenga kuwasaidia wajasiriamali kujenga biashara zenye mpangilio, uimara na uwezo wa kukua. Juhudi hizi zinaakisi safari ya zaidi ya miaka 30 ya Stanbic Bank ya kukua pamoja na Watanzania kwa kuwekeza kwa watu, jamii na biashara zinazochangia maendeleo ya kila siku.

Akizungumza katika tukio hilo, Mkuu wa Biashara Incubator kutoka Stanbic Bank Tanzania, Kai Mollel, alisema Mama na Baba Lishe wana mchango mkubwa katika maisha ya jamii na uchumi wa maeneo yao.

Mkuu wa Kitengo cha Biashara Incubator Benki ya Stanbic, Kai Mollel akitoa elimu kwa akinamama lishe na babalishe Mkoa wa Dodoma wakati wa mafunzo ya ujasiriamali wa chakula yaliyoandaliwa na benki hiyo Jijini Dodoma

“Mama na Baba Lishe si wajasiriamali wa kawaida katika uchumi wetu. Wao hulisha jamii, hutegemeza familia, hujenga kipato cha kila siku na huchangamsha masoko ya maeneo yao. Kupitia RISE Mama Lishe, tunawasaidia kutoka katika biashara za kujikimu pekee na kuelekea katika biashara imara, salama na zenye mpangilio bora zaidi,” alisema Mollel.

Mollel aliongeza kuwa tukio la Dodoma linaonyesha imani ya Stanbic Bank kuwa ukuaji jumuishi lazima uwafikie wajasiriamali wanaochochea uchumi wa kila siku katika jamii.

“Jiko banifu ni zaidi ya kifaa cha kupikia. Kwa mfanyabiashara wa chakula, linaweza kupunguza gharama za nishati, kupunguza moshi, kuboresha usalama wa mazingira ya kazi na kuweka msingi bora wa ukuaji. Huu ndiyo msaada wa vitendo unaobadilisha namna biashara ndogo zinavyoendeshwa kila siku. Tunapoendelea kuadhimisha zaidi ya miaka 30 ya kukua pamoja na Watanzania, lengo letu linabaki kuwa kuleta suluhisho zinazogusa maisha ya watu na kuwasaidia kujenga maisha bora pamoja na biashara imara,” alisema.

Meneja Miradi kutoka GIZ, Lisa Zschunke, alisema ushirikiano huo unalenga kuleta mabadiliko ya vitendo kwa wajasiriamali wa biashara za chakula, huku ukiunga mkono ajenda ya Taifa ya nishati safi ya kupikia.

“RISE Mama Lishe inaonyesha namna ukuaji wa biashara na matumizi ya nishati safi ya kupikia vinavyoweza kwenda pamoja katika kuboresha maisha ya wajasiriamali. Kwa kuwapatia wanawake na vijana wajasiriamali mafunzo ya biashara pamoja na majiko banifu, tunachangia mazingira salama zaidi ya kazi, usimamizi bora wa gharama na uimara wa biashara ndogo. Ushirikiano huu unaonyesha dhamira yetu ya pamoja ya kuleta suluhisho za vitendo zinazogusa jamii na kuchangia lengo la Tanzania la matumizi ya nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2032,” alisema Zschunke.

Mafunzo ya RISE Mama Lishe yanahusisha mtazamo wa ujasiriamali, upangaji wa biashara, upangaji wa bei, usimamizi wa fedha, huduma kwa wateja, usafi na usalama wa chakula, matumizi ya mifumo ya kidijitali katika biashara pamoja na uelewa wa nishati safi ya kupikia. Mtazamo huu unawapa wajasiriamali maarifa wanayoweza kuyatumia moja kwa moja katika biashara zao, huku ugawaji wa majiko banifu ukiimarisha usalama na ufanisi katika shughuli zao za kila siku.

Kupitia Stanbic Biashara Incubator, Stanbic Bank inaendelea kutoa jukwaa linalowasaidia wajasiriamali kujenga biashara imara, kupata maarifa, kuimarisha nidhamu ya biashara na kujiandaa kwa ukuaji wa muda mrefu. Programu hii pia inaonyesha mchango mpana wa benki katika kukuza biashara zinazoongozwa na wanawake na vijana, kuongeza kipato cha kaya, kuchochea ajira na kupanua ushiriki wa Watanzania katika uchumi jumuishi.

Hii pia inaendana na imani ya Stanbic Bank kuwa Tanzania ni nyumbani, na benki ina jukumu la kuchangia ukuaji wake kwa kuwaunga mkono watu, biashara na jamii zinazolisukuma Taifa mbele kila siku. Kupitia RISE Mama Lishe, dhamira hii inageuzwa kuwa vitendo kwa kuwekeza katika ukuaji wa wajasiriamali, matumizi ya nishati safi ya kupikia na ushiriki mpana zaidi katika maendeleo ya uchumi.

RISE Mama Lishe inapofika Dodoma, Stanbic Bank na GIZ zinathibitisha tena dhamira yao ya kuimarisha biashara za ndani, kuunga mkono matumizi ya nishati safi ya kupikia na kuleta thamani ya vitendo na endelevu kwa wanawake na vijana wajasiriamali nchini.

Leave a Comment