×

Polisi Wafunguka Sakata la David Jumbe Uchunguzi Bado Unaendelea

Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limetoa taarifa kuhusu sakata la David Joseph Mghanja maarufu Djumbe, kufuatia taarifa zilizosambaa mitandaoni zikidai alikamatwa na watu wasiojulikana usiku wa Mei 20, 2026.

Kupitia taarifa iliyotolewa na Kaimu Kamanda wa Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam, SACP Faustine Mafwele, Jeshi la Polisi limesema linaendelea na uchunguzi wa tukio hilo ili kubaini mazingira halisi ya kilichotokea pamoja na watu waliohusika.

Kwa mujibu wa Polisi, tayari wamefanikiwa kulipata gari aina ya Toyota Wish lenye namba T 609 DTD, rangi nyeusi, ambalo linadaiwa kumilikiwa na Allan Elisonguo Macha. Polisi wanadai kuwa Djumbe alikuwa mmoja wa abiria ndani ya gari hilo wakati wa tukio linalodaiwa kuwa la kukamatwa kwake maeneo ya Bunju.

Aidha, taarifa hiyo imeeleza kuwa asubuhi ya Mei 21, 2026, Jeshi la Polisi lilipokea taarifa zikidai kuwa Djumbe alikuwa katika ofisi za Chadema zilizopo Mikocheni, lakini askari walipofika eneo hilo hawakumkuta.

Polisi wameeleza kuwa Djumbe tayari amepatikana salama na kwamba uchunguzi bado unaendelea ili kuwabaini watu waliomkamata pamoja na sababu za tukio hilo kabla ya hatua za kisheria kuchukuliwa dhidi ya watakaohusika.

Tukio hilo limeendelea kuzua mjadala mkubwa mitandaoni na katika duru za kisiasa huku wadau mbalimbali wakisubiri taarifa rasmi zaidi kutoka kwa mamlaka husika.

Leave a Comment