
Dar es Salaam, Tanzania – 21 May 2026: Benki ya Exim Tanzania hii leo imezindua huduma yake ya Exim WhatsApp Banking, suluhisho jipya la kidijitali lililobuniwa kufanya huduma za kibenki za kila siku kuwa za haraka, rahisi na zinazofikika kwa kupitia jukwaa la WhatsApp.
Huduma hii inawawezesha wateja kupata huduma mbalimbali za kibenki moja kwa moja kupitia WhatsApp. Huduma hizo ni pamoja na kuangalia salio, kuhamisha fedha, kutuma fedha kwenda simu za mkononi, kufanya malipo kwa wafanyabiashara, kulipia huduma za serikali kupitia GePG, pamoja na huduma zinazohusiana na kadi za benki. Mteja anaweza kupata huduma zote hizi kupitia jukwaa la WhatsApp bila uhitaji wa kupakua programu nyingine yoyote wala haja ya kutembelea tawi la benki.
Mkuu wa Kitengo cha Mifumo Mbadala ya kidigitali wa Benki ya Exim, Bw Silas Matoi, akizungumza wakati wa uzinduzi, amesema mfumo huu umebuniwa kwa ajili ya kurahisisha upatikanaji wa huduma za kibenki na kuimarisha ubora wa huduma kwa wateja.
‘‘Kupitia Exim WhatsApp Banking, wateja wetu sasa wanaweza kuangalia salio kwenye akaunti zao, kutuma fedha kwenda kwenye mitandao ya simu, kulipa bili na malipo mbalimbali ya serikali, kupata huduma zote zinazohusiana na kadi, pamoja na kufanya miamala mingine moja kwa moja kupitia WhatsApp. Hii inaondoa ulazima wa aidha kupakua, kubadilisha programu mbalimbali au kupitia mifumo migumu, kwani sasa huduma zote muhimu za kibenki zinapatikana sehemu moja, iliyozoeleka, rahisi na inayopatikana kwa watu wote” Alisema Silas.
Katika hatua nyingine, bwana Matoi, ameeleza kuhusu ubora wa teknolojia iliyotumika kubuni mfumo huu na hakikisho la usalama.
“Tumejenga suluhisho hili huku tukizingatia misingi ya usalama na urahisi wake. Wateja wetu wasiwe na wasiwasi, wanaweza kufanya miamala kwa kujiamini wakijua kuwa kila mawasiliano yanalindwa kupitia mifumo salama ya uthibitishaji ikiwemo uthibitisho wa PIN. Wakati huo huo, mfumo huu unasalia kuwa rahisi, wa haraka na mwepesi kutumia, kwa sababu lengo kubwa ni kufanya huduma za benki kidijitali ziwe za kawaida na zinazofikika kwa kila mteja,” Amesema Matoi.
Huduma hii mpya ya Exim WhatsApp Banking, inawawezesha wateja wa Benki ya Exim kufanya miamala yao ya kila siku kupitia jukwaa hilo wanalolitumia kila siku, hivyo kuondoa ulazima wa kupakua aplikesheni nyingine tofauti huku wakifurahia huduma za kibenki zilizo rahisi, za haraka na zilizozoeleka.
Kwa upande wake Meneja Mkuu wa masoko na Mawasiliano wa Exim Benki Tanzania, Kauthar D’souza, akizungumzia umuhimu wa uzinduzi wa mfumo huu, amesema kuanzishwa kwa huduma ya Exim WhatsApp Banking kunadhihirisha dhamira endelevu ya benki hiyo katika kuleta ubunifu na kuboresha huduma kwa wateja.
“Wateja wetu tayari wanatumia WhatsApp kila siku kwa mawasiliano yao, kufanya biashara na kusimamia shughuli zao za kila siku. Kwa kuleta huduma za benki ndani ya mazingira hayo hayo, tunafanya huduma za kifedha kuwa rahisi kufikiwa, kueleweka na kutumika kwa urahisi zaidi. Mteja wetu hapaswi kujifunza mfumo mpya au kupakua aplikesheni nyingine ili tu kuangalia salio lako au kulipa bili. Huduma za benki zinapaswa kufanyika kulingana na namna unavyoishi na kufanya kazi, na si vinginevyo” Amesema Kauthar
“Uzinduzi huu ni sehemu ya mikakati yetu mipana ya kuendelea kuleta ubunifu unaochochewa na mahitaji halisi ya wateja wetu na kuendana na kasi ya mabadiliko ya teknolojia. Tunazingatia namna wateja wetu wanavyoishi, tunaelewa mifumo na majukwaa wanayoyaamini, na kisha tunabuni suluhisho rahisi linaloendana na maisha yao ya kila siku. Huduma ya Benki kupitia WhatsApp si tu njia mpya ya kutoa huduma, bali pia hatua inayodhihirisha kuwa benki ya Exim ni benki inayokua sambamba na wateja wake, inayosikiliza mahitaji yao, na kufanya maisha yao ya kifedha kuwa rahisi zaidi kila siku”
Wateja wanaweza kupata huduma hii kwa kuanzisha mawasiliano kwa njia ya ujumbe kupitia namba rasmi ya WhatsApp ya Benki ya Exim Tanzania [+255 675 800 100], ambapo wataelekezwa kupitia mchakato rahisi wa usajili ikiwemo kuweka PIN, kabla ya kuanza kutumia huduma mbalimbali zinazopatikana.
Benki ya Exim pia ina mpango wa kupanua huduma hii kwa kuongeza vipengele vingine ikiwemo maombi ya mikopo na huduma za uwekezaji, ikiwa ni sehemu ya mkakati wake endelevu wa mageuzi ya kidijitali.