×

Trump Afichua Mwanga Wa Amani Kati Ya Marekani Na Iran

Marekani chini ya Donald Trump na Iran zinaonekana kukaribia makubaliano muhimu ya amani ambayo yanaweza kufungua tena Mlango wa Bahari wa Hormuz, eneo muhimu sana kwa usafirishaji wa mafuta duniani.

Trump amesema kupitia Truth Social kuwa sehemu kubwa ya makubaliano hayo tayari imekubaliwa, huku maelezo ya mwisho yakitarajiwa kutangazwa muda wowote. Makubaliano hayo yanatajwa kulenga kumaliza rasmi vita vilivyoanza Februari kati ya Marekani, Israel na Iran, pamoja na kurejesha usafirishaji wa kawaida wa mafuta kupitia Hormuz.

“Tumemaliza mazungumzo mazuri sana na Rais Mohammed bin Salman Al Saud wa Saudi Arabia, Mohammed bin Zayed Al Nahyan wa Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), Emir Tamim bin Hamad bin Khalifa Al Thani, Waziri Mkuu Mohammed bin Abdulrahman bin Jassim bin Jaber Al Thani pamoja na Waziri Ali al-Thawadi wa Qatar, Field Marshal Syed Asim Munir Ahmed Shah wa Pakistan, Rais Recep Tayyip Erdoğan wa Türkiye, Rais Abdel Fattah El-Sisi wa Misri, Mfalme Abdullah II wa Jordan na Mfalme Hamad bin Isa Al Khalifa wa Bahrain kuhusu Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na masuala yote yanayohusiana na Waraka wa Makubaliano kuhusu AMANI.” amesema Rais wa Marekani Donald Trump amesema 

Makubaliano hayo yanatajwa kuwa hatua muhimu ya kumaliza mzozo mkubwa kati ya Marekani, Israel na Iran uliodumu kwa miezi kadhaa na kuathiri uchumi pamoja na bei ya mafuta duniani.

Kwa mujibu wa taarifa mbalimbali, makubaliano hayo yatahusisha:

  • Kufunguliwa tena kwa Strait of Hormuz
  • Kuondolewa kwa baadhi ya vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran
  • Iran kuruhusiwa kuuza mafuta yake kwa uhuru zaidi
  • Mazungumzo mapya kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran ndani ya siku 30 hadi 60

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubio amesema dunia inaweza kupata habari njema ndani ya saa chache zijazo kuhusu mzozo huo.

Iran imeendelea kusisitiza kuwa mpango wake wa nyuklia ni kwa matumizi ya kiraia pekee, huku Marekani ikitaka kuhakikisha Iran haitengenezi silaha za nyuklia.

Katika hatua nyingine, vyombo vya habari vya Iran vimeripoti kuwa makubaliano hayo pia yatazuia Marekani na washirika wake kushambulia Iran, huku Iran nayo ikiahidi kutofanya mashambulizi ya awali dhidi ya Marekani au washirika wake.

Hata hivyo, bado kuna tofauti kadhaa ambazo hazijatatuliwa kikamilifu. Iran inataka:

  • Marekani iondoe vizuizi vya bandari zake
  • Fedha zake zilizogandishwa duniani zirejeshwe
  • Hakikisho kuwa hakutakuwa na mashambulizi mapya

Kwa upande mwingine, mwanasiasa wa Israel Benny Gantz ameonya kuwa Israel haipaswi kukubali makubaliano yoyote yatakayoweka usitishaji wa mapigano Lebanon bila kulinda usalama wa mipaka yake.

Leave a Comment