×

Ghetto Kids Kutinga Kombe la Dunia 2026 Kupitia Mwaliko wa Shakira

Kundi maarufu la watoto wa dansi kutoka Uganda, Ghetto Kids, limeendelea kuvuta hisia duniani baada ya kupata nafasi ya kushiriki kwenye halftime show ya fainali ya Kombe la Dunia 2026 kupitia mwaliko maalum kutoka kwa Shakira.

Kupitia ukurasa wake wa Instagram wiki iliyopita, Shakira aliwatangaza rasmi watoto hao kama kundi la kwanza alilolichagua kushiriki naye katika burudani ya fainali ya Kombe la Dunia itakayofanyika nchini Marekani, Canada na Mexico msimu huu wa joto. Tangazo hilo limeibua furaha kubwa kwa watoto hao ambao walitokea mitaa ya Kampala kabla ya kuwa gumzo duniani kupitia vipaji vyao vya kucheza.

Kundi hilo ambalo lilianzishwa kama sehemu ya NGO inayosaidia watoto wa mitaani na yatima kupitia sanaa na dansi, limekuwa likipata umaarufu mkubwa kutokana na video zao za kucheza zilizokuwa zikisambazwa mitandaoni. Umaarufu wao uliwahi kuwafungulia milango hadi kushiriki kwenye kipindi maarufu cha America’s Got Talent.

Mmoja wa watoto hao mwenye umri wa miaka minane, Busingye Josephine Daniella, amesema wana hamu kubwa ya kuonyesha dunia kile wanachoweza kufanya. Kwa upande wake, Ssegirinyi Madwanah mwenye miaka 16 amesema kupata nafasi ya kusafiri nje ya Uganda na kutumbuiza kwenye moja ya majukwaa makubwa duniani ni fursa kubwa ambayo inaweza kubadilisha maisha yao.

Mwanzilishi wa Ghetto Kids, Kavuma Dauda ambaye naye aliwahi kuishi mtaani, amesema ana matumaini kuwa nafasi hiyo itasaidia kundi hilo kupata ufadhili zaidi kwa ajili ya kujenga kituo cha elimu na kuwasaidia watoto wengine wenye mazingira magumu.

Ushirikiano huo kati ya Shakira na Ghetto Kids tayari umeanza kuwafanya watoto hao kuwa gumzo duniani huku wengi wakisifu namna vipaji vya Afrika vinaendelea kupata nafasi kwenye majukwaa makubwa ya kimataifa.

Leave a Comment