
Mwanamke mmoja mkazi wa Kibera nchini Kenya, Maureen Masili, amelazwa katika Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta baada ya kudaiwa kushambuliwa na kuchomwa kwa maharagwe ya moto kufuatia mabishano ya kisiasa yanayohusishwa na kumuunga mkono Rais wa Kenya William Ruto.
Kwa mujibu wa familia yake, tukio hilo lilitokea Mei 18, 2026 wakati wa maandamano yaliyokuwa yakifanyika Nairobi kupinga kupanda kwa bei ya mafuta. Inadaiwa kuwa mabishano yalizuka baada ya Masili kuonyesha kuunga mkono harakati ya “Tutam”, inayohamasisha muhula wa pili wa Ruto kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2027.
Akizungumza akiwa hospitalini, Masili alisema msimamo wake wa kisiasa ndio chanzo cha shambulio hilo. Dada yake, Lilian Kakuli, amesema mshambuliaji alikasirishwa na kauli za kuunga mkono serikali kabla ya kwenda katika kibanda cha chakula na kuchukua maharagwe yaliyokuwa yanachemka na kuyamwaga juu yake.
Familia hiyo imesema Masili ameungua vibaya katika maeneo mbalimbali ya mwili wake ikiwemo kifua, tumbo, mapaja pamoja na sehemu za siri, huku madaktari wakieleza kuwa baadhi ya maeneo yameathirika kwa kiwango kikubwa.
Kesi hiyo imeripotiwa katika Kituo cha Polisi cha Kibera huku Kamanda wa Polisi wa Kilimani, Patricia Yegon, akithibitisha kuwa Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) imeanza uchunguzi wa tukio hilo na inaendelea kuwatafuta mashahidi muhimu.
Familia ya Masili sasa imeitaka serikali ya Kenya kuchukua hatua dhidi ya ongezeko la chuki na kutovumiliana kisiasa nchini humo kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2027.
Tukio hilo limeibua mjadala mkubwa nchini Kenya, likija wiki chache baada ya mwanamuziki wa nyimbo za injili Rachel Wandeto kufariki dunia kutokana na majeraha ya kuungua katika tukio jingine lililodaiwa kuhusishwa na msimamo wake wa kisiasa pamoja na kumuunga mkono Rais Ruto.