×

Meta Yazindua Huduma za Kulipia Kwa Facebook, Instagram na WhatsApp

Kampuni ya teknolojia ya Meta imetangaza rasmi kuzindua huduma mpya za usajili wa kulipia kwa majukwaa yake ya Facebook, Instagram pamoja na WhatsApp, hatua inayotajwa kubadili kwa kiasi kikubwa mfumo wa mapato wa kampuni hiyo ambao kwa muda mrefu ulitegemea matangazo.

Huduma hizo mpya zinajulikana kama “Plus” na zitawapa watumiaji vipengele vya ziada vya ubinafsishaji, kuongeza uonekano wa machapisho pamoja na zana maalumu za ushirikishwaji wa hadhira.

Kwa mujibu wa Meta, huduma ya Instagram Plus na Facebook Plus zitagharimu dola 3.99 kwa mwezi kila moja, huku WhatsApp Plus ikigharimu dola 2.99 kwa mwezi.

Instagram Plus itakuwa na vipengele vipya kama kuongeza muda wa kuonekana kwa Instagram Stories zaidi ya saa 24, uwezo wa kuona mara ambazo Story imetazamwa tena, kuangalia Stories kwa siri bila kuonekana kwenye orodha ya waliotazama pamoja na kuangaziwa kwa Stories kila wiki.

Watumiaji pia watapata zana za kubinafsisha akaunti zao ikiwemo fonti maalumu, ikoni tofauti za programu, pini za ziada kwenye wasifu pamoja na miitikio maalumu ya “Super Heart”.

Kwa upande wa Facebook Plus, huduma hiyo italenga zaidi kuongeza ushirikishwaji wa hadhira pamoja na ubinafsishaji wa wasifu wa watumiaji.

WhatsApp Plus yenyewe italeta vipengele vipya vya ujumbe na muonekano wa programu, ikiwemo sauti maalumu za arifa, mandhari tofauti za WhatsApp, stika za kipekee, uwezo wa kubandika mazungumzo mengi zaidi pamoja na zana za kupanga mawasiliano.

Meta imesema huduma hizi mpya hazitachukua nafasi ya huduma yake ya sasa ya Meta Verified ambayo inalenga uthibitisho wa akaunti, ulinzi dhidi ya watu wanaojifanya wengine pamoja na huduma kwa wateja.

Hatua hiyo inakuja wakati kampuni hiyo inaendelea kuongeza uwekezaji mkubwa katika teknolojia ya akili unde (AI), ambapo Meta inakadiriwa kutumia hadi dola bilioni 145 mwaka huu kwa ajili ya vituo vya data na miundombinu ya AI.

Wakati huohuo, kampuni hiyo inaendelea kujaribu huduma nyingine mpya ya usajili ijulikanayo kama “Meta One” inayolenga watengenezaji wa maudhui, biashara pamoja na watumiaji wa Meta AI.

Kwa kufanya hivyo, Meta sasa inaungana na kampuni nyingine za mitandao ya kijamii kama Snapchat na X ambazo tayari zina huduma za usajili wa kulipia kwa watumiaji wake.

Leave a Comment