
Mchezaji wa zamani wa timu ya Timu ya Uingereza, Raheem Sterling amekamatwa na polisi kufuatia ajali aliyopata akiwa anaendesha gari lake la kifahari aina ya Lamborghini kwenye barabara kuu ya M3 nchini Uingereza .
Tukio hilo lilitokea Alhamisi asubuhi katika eneo la Hampshire ambapo gari la nyota huyo lilidaiwa kugonga vizuizi vya pembeni mwa barabara.
Polisi walifika eneo la tukio muda mfupi baadaye na kumkamata Sterling kwa tuhuma mbalimbali ikiwemo kuendesha gari akiwa chini ya ushawishi wa dawa za kulevya, kuendesha kwa hatari pamoja na kushindwa kutoa sampuli ya uchunguzi.
Kwa mujibu wa taarifa ya polisi, hakuna majeruhi walioripotiwa katika ajali hiyo na hakukuwa na gari jingine lililohusika.

Baada ya mahojiano, Sterling aliachiwa kwa dhamana huku uchunguzi zaidi ukiendelea kufanyika.
Nyota huyo mwenye miaka 31 kwa sasa anakitumikia kikosi cha Feyenoord baada ya kuachana na Chelsea F.C. mapema mwaka huu. Kabla ya hapo aliwahi kung’ara akiwa na klabu za Liverpool F.C. na Manchester City F.C. ambapo alitwaa mataji kadhaa makubwa ikiwemo Ligi Kuu England.
Sterling pia aliwahi kuwa mmoja wa wachezaji muhimu wa timu ya Timu ya Uingereza akicheza mechi 82 na kufunga mabao 20 katika kipindi chake cha kimataifa.