
Rais wa Romania Nicușor Dan ameitisha kikao cha dharura cha baraza kuu la ulinzi wa taifa kufuatia kile alichokitaja kuwa tukio kubwa zaidi kuikumba nchi hiyo tangu kuanza kwa vita kati ya Russia na Ukraine.
Hatua hiyo imekuja baada ya ndege isiyo na rubani inayodaiwa kutoka Urusi kugonga jengo la ghorofa katika mji wa Galati karibu na mpaka wa Ukraine, na kusababisha watu wawili kujeruhiwa kwa mujibu wa Wizara ya Ulinzi ya Romania.
Rais Nicușor Dan amesema serikali yake inatafuta msaada wa ziada kutoka kwa washirika wake ili kuimarisha uwezo wa kukabiliana na mashambulizi ya ndege zisizo na rubani.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa NATO Mark Rutte amelaani tukio hilo akilitaja kuwa ni tabia ya hatari na ya kutojali kutoka upande wa Urusi.

Rutte ameihakikishia Romania kuwa NATO iko tayari kulinda kila eneo la nchi wanachama wake huku akisisitiza kuwa muungano huo utaendelea kuimarisha ulinzi wake pamoja na kuiunga mkono Ukraine dhidi ya mashambulizi ya Urusi.
Katika hatua nyingine, Romania imemfukuza balozi wa Urusi nchini humo na kufunga ubalozi wa Urusi baada ya mashambulizi hayo ya ndege zisizo na rubani katika eneo la makazi.
Serikali ya Romania imemtangaza balozi huyo wa Urusi kuwa “mtu asiyekubalika” ndani ya taifa hilo.
Kwa upande wa Urusi, msemaji wa Kremlin amesema Vladimir Putin amepatiwa taarifa kuhusu tukio hilo, huku vyombo vya habari vya Urusi vikieleza kuwa Moscow itajibu hatua ya Romania ya kumfukuza balozi wake.