
Jeshi la Israel limekamata eneo la kimkakati la Ngome ya Beaufort kusini mwa Lebanon, katika hatua ambayo Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu ameieleza kuwa ni “mabadiliko ya kuamua” katika operesheni yake dhidi ya Hezbollah.
Hatua hii imekuja wakati vikosi vya ardhini vinaendelea kupenya zaidi ndani ya ardhi ya Lebanon, vikivuka mpaka wao wa awali uliowekwa kwenye Mto Litani.
Wakati huo huo, Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) limepanua eneo la kusini mwa Lebanon ambalo limewaonya wakazi wake kuondoka.
Waziri Mkuu wa Lebanon ameishutumu Israel kwa kutekeleza “adhabu ya pamoja.”
Ikiwa juu ya Bonde la Litani, Ngome ya Beaufort imekuwa muhimu katika kudhibiti eneo linaloizunguka tangu ilipojengwa na wanajeshi wa Vita vya Msalaba takribani miaka 900 iliyopita. Jeshi la Israel liliikamata mara ya kwanza miaka 44 iliyopita katika vita vinavyojulikana nchini Israel kama Vita ya Kwanza ya Lebanon.
Katika taarifa yake Jumapili baada ya kuikamata tena, Netanyahu alisema ni “hatua ya kuamua na mabadiliko makubwa katika sera yetu.”
“Tumevunja kizuizi cha hofu. Sasa tunachukua hatua, tunafanya operesheni katika maeneo yote Syria, Gaza, Lebanon,” alisema.
Netanyahu aliongeza kuwa lengo lake ni “kuimarisha na kupanua udhibiti wetu katika maeneo yaliyokuwa chini ya Hezbollah.”
Waziri wa Ulinzi Israel Katz alikumbusha mapigano ya miaka 44 iliyopita dhidi ya Shirika la Ukombozi wa Palestina (PLO), mojawapo ya mapigano ya mwanzo ya vita vya Lebanon. Alisema Brigedi ya Golani, iliyouteka wakati huo, imerudi na kupandisha bendera ya Israel juu yake.
Hivyo basi, kwa mtazamo wa Israel, huu ni ushindi wenye umuhimu mkubwa wa kimkakati na pia wa kiishara.
🔴 Tufuatilie kupitia YouTube ya Global TV, like, comment ili kuendelea kuhabarika kila siku kwa habari mbalimbali zenye ukweli na uhakika.