
Serikali ya Kuwait imeishutumu Iran kwa kile ilichokiita mashambulizi ya mara kwa mara na ya kinyama, ikisema kuwa hatua hiyo ni hatari kubwa kwa usalama na utulivu wa taifa hilo pamoja na eneo lote la Ghuba.
Kupitia taarifa iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Nje ya Kuwait, nchi hiyo ilisema mashambulizi hayo ni ongezeko hatari la mzozo na yanahatarisha maisha ya raia pamoja na miundombinu muhimu ya taifa.
Taarifa hiyo imeongeza kuwa kuendelea kwa mashambulizi hayo kunadhoofisha juhudi za kupunguza mvutano wa kisiasa na kijeshi katika ukanda huo.
Mapema Jumatatu, mifumo ya ulinzi wa anga ya Kuwait ilifanikiwa kudungua makombora na droni kadhaa huku ving’ora vya tahadhari vikisikika katika maeneo mbalimbali ya nchi hiyo.
Kwa upande wake, Saudi Arabia nayo ililaani vikali mashambulizi hayo kupitia Wizara yake ya Mambo ya Nje, ikisema kuwa yanakiuka sheria za kimataifa pamoja na Mkataba wa Umoja wa Mataifa.
“Ufalme wa Saudi Arabia unakataa kabisa mashambulizi haya yanayokiuka mamlaka ya Kuwait na kuhatarisha juhudi za kurejesha amani na usalama katika ukanda huu,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo.
Nayo Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) ulitoa tamko ukiyataja mashambulizi hayo kama mashambulizi ya kigaidi ya Iran dhidi ya Kuwait.
Katibu Mkuu wa Baraza la Ushirikiano la Ghuba (GCC), Jasem Mohamed Al-Budaiwi, amesema mashambulizi hayo ni hatua hatari na isiyokubalika inayovunja mamlaka ya Kuwait.
Wakati huo huo, Jeshi la Kuwait limewataka wananchi kufuata maelekezo ya kiusalama yanayotolewa na mamlaka husika.
Kwa upande mwingine, Kikosi Maalum cha Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran (IRGC) kilisema kuwa kikosi chake cha anga kililenga kambi ya kijeshi iliyotumika katika kile walichodai kuwa ni shambulio la Marekani dhidi ya mnara wa mawasiliano katika Kisiwa cha Sirik, ingawa hakikufafanua eneo halisi la kambi hiyo.
Wiki iliyopita, Kuwait pia ilikumbwa na mashambulizi ya droni na makombora ambayo iliilaumu Iran, ikiyataja kuwa ni hatua nyingine ya hatari inayoongeza mvutano katika eneo la Mashariki ya Kati.