
Studio za msanii wa Bongo Fleva, Barnaba Classic, zimeteketea kwa moto usiku wa kuamkia Juni 1, 2026 katika eneo la Mwananyamala jijini Dar es Salaam, tukio ambalo limesababisha hasara kubwa ya vifaa na mali zilizokuwa ndani ya studio hizo.
Akizungumza na Global TV baada ya tukio hilo, Barnaba Classic amesema moto huo ulianza ghafla wakati akiwa hajafika eneo la tukio, hali iliyomfanya kupata taarifa za mshutuko mkubwa kutoka kwa watu waliokuwa karibu.
Amesema hadi sasa chanzo cha moto huo bado hakijafahamika, huku akieleza kuwa vifaa muhimu vya muziki, miradi ya nyimbo pamoja na vifaa vya kazi vimeteketea kabisa.
Barnaba ameongeza kuwa hasara iliyotokea ni kubwa kwa kuwa studio hizo zilikuwa sehemu muhimu ya kazi zake za muziki na maendeleo ya wasanii wengine aliokuwa akiwasaidia.
Vikosi vya zimamoto na uokoaji vilifika eneo la tukio na kufanikiwa kudhibiti moto huo baada ya jitihada kubwa, ingawa uharibifu tayari ulikuwa umeshatokea.
Polisi wamesema uchunguzi unaendelea kubaini chanzo cha moto huo, huku msanii huyo akiomba msaada na ushirikiano katika kipindi hiki kigumu.