
Pweza ni kiumbe cha baharini chenye maajabu mengi ikiwemo kuwa na mioyo 3 ambapo moyo mmoja husukuma damu kwenda sehemu mbalimbali za mwili na mioyo 2 husukuma damu kupitia matamvua yake.
Tofauti na viumbe wengine wenye damu nyekundu, Pweza ana damu ya rangi ya bluu kwa sababu ana “copper-based protein”.
Pweza ni miongoni mwa viumbe wenye akili zaidi duniani, mstaarabu na msafi. Anayo mikia au mikono nane na macho mawili makubwa. Jamii za samaki pweza ni zaidi ya jamii 289 kulingana na chapisho la World Animal Foundation.
Pweza wa kawaida huwa anakuwa na urefu wa inchi 12-36 na uzito wa kilo 3-10. Pweza mkubwa zaidi duniani anapatikana katika Bahari ya Pacific, jamii ya Enteroctopus dofleini anakuwa mkubwa hadi mita 5 urefu na kilo hadi 50 kwa mujibu wa World animal foundation.

Pweza anakula nyama tu (carnivores), hupendelea kula jamii ya dagaa kamba (uduvi) na samaki, akiwinda kwa kutumia mikono yake nane.
Pweza anauwezo wa kubadili rangi kama kinyonga kulingana na mazingira aliyopo, unaweza kubadilika katika rangi tafauti kama kuwa rangi ya bluu, pinki, rangi ya ugoro au kijani ili kujificha na kufanana na mazingira yaliyomzunguka kutokana na maadui.
Pweza pia humwaga wino na kukimbia kwa kasi sana na kumfanya adui asimuone kwa sababu ya maji kuchanganyikana na wino na kufanya hali kama ukungu.

Uzalianaji wa pweza huwa ni wa kutaga mayai na kuyalinda mpaka kutotolewa. Pweza ni kiumbe asiyekuwa na wivu wa kimapenzi, jike moja hupandwa na madume zaidi ya 10 wakiwa wamemzunguka kwa kuweka duara na kumuweka katikati kisha madume kuachiana zamu ya kujamiiana.
Pweza dume huwa na mkono mmoja kati ya 8 mahususi kwa kupitisha mbegu za uzazi. Pweza dume baada ya kumaliza kujamiiana na jike hukaa muda mfupi na kufa kwa sababu huwa anamaliza akili na nguvu za kutafuta chakula na hatimaye kuishiwa nguvu na kufa.
Pweza jike ana uwezo wa kutaga mayai Zaidi ya (200,000 – 400,000) inategemeana na jamii ya pweza. Pweza jike hulalia na kulinda mayai mpaka mayai yatotolewe au kuanguliwa pia huwalinda watoto wake kwa muda mpaka wakue.
Makala na Elvan Stambuli, Global Digital