×

Kiungo wa Serengeti Boys Aibuka Mfungaji Bora Mashindano ya AFCON U17

Mchezaji Serengeti Boys, Dismas Athanasi ameshinda tuzo ya mfungaji bora wa mashindano ya AFCON U17

Kiungo wa Serengeti Boys, Dismas Athanasi, ameibuka mfungaji bora wa michuano ya Kombe la Mataifa Afrika kwa vijana chini ya miaka 17 (AFCON U-17) baada ya kufunga jumla ya mabao matatu katika mashindano hayo.

Athanasi amefanya vyema na kuisaidia Tanzania kumaliza katika nafasi ya pili, baada ya Serengeti Boys kupoteza fainali kwa mikwaju ya penalti 4-2 dhidi ya Senegal, ambao ndio mabingwa wapya wa michuano hiyo.

Licha ya kupoteza ubingwa, Serengeti Boys wameondoka na heshima kubwa baada ya kutwaa medali za fedha kama washindi wa pili, hatua inayotajwa kuwa mafanikio makubwa kwa soka la vijana Tanzania.

Katika tuzo nyingine, Serengeti Boys imetunukiwa tuzo ya timu yenye nidhamu bora (Best Fair Play), ikionesha nidhamu na mchezo wa kiungwana waliouonesha katika mashindano yote.

Kwa upande wa tuzo za binafsi, golikipa wa Senegal, Assane Sarr, ameibuka mshindi wa tuzo ya golikipa bora wa michuano hiyo kutokana na kiwango chake bora kilichosaidia timu yake kutwaa ubingwa.

Leave a Comment