
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amerejea nchini leo Juni 6, 2026 akitokea jijini St. Petersburg nchini Urusi alipokuwa katika ziara ya kitaifa ya kikazi kwa mwaliko wa Rais wa Urusi, Vladimir Putin.
Mara baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) jijini Dar es Salaam, Rais Samia alipokelewa na Makamu wa Rais, Dkt. Emmanuel John Nchimbi pamoja na Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dkt. Asha-Rose Migiro na viongozi wengine wa Serikali na chama.

Akiwa nchini Urusi, Rais Samia alishiriki katika Jukwaa la Kimataifa la Uchumi la St. Petersburg (SPIEF) pamoja na kufanya mazungumzo ya kidiplomasia na viongozi mbalimbali kuhusu ushirikiano wa kiuchumi, biashara, uwekezaji na maendeleo kati ya Tanzania na Urusi.
Ziara hiyo imeelezwa kuwa sehemu ya juhudi za Tanzania kuimarisha diplomasia ya uchumi na kuvutia wawekezaji katika sekta mbalimbali muhimu ikiwemo nishati, miundombinu, utalii na biashara.

