
Bondia wa Tanzania, Hassan Mwakinyo, amepoteza pambano lake la ubingwa dhidi ya Michel Soro kwa TKO katika raundi ya tisa, katika pambano lililofanyika Abidjan, Ivory Coast usiku wa kuamkia leo Juni 11, 2026.
Mwakinyo alikuwa akiwania mkanda wa IBO katika uzito wa Middleweight wa raundi 12, lakini ndoto hiyo ilizimika baada ya mwamuzi kusimamisha pambano kutokana na presha kubwa kutoka kwa mpinzani wake, Michel Soro.
Baada ya pambano hilo, Mwakinyo alitoa ujumbe wa pole kwa mashabiki wake akikiri kuwa hakufanya vizuri kama ambavyo wengi walivyotarajia, akieleza kuwa hali yake ya kimwili ilimuathiri ulingoni.

“Napenda nitoe pole za maumivu kwa wote mlioumizwa au kutokuelewa kilichotokea jana. Siamini katika matokeo ya kupoteza kwangu, lakini siumii sana kwa sababu ndio mchezo. Kinachoniumiza zaidi ni kuwa nilikuwa weak kiasi cha kushindwa kujitetea. Hata namna ya upiganaji wangu haikuwa ile mliyoizoea,” alisema Mwakinyo.
Ameongeza kuwa alijiandaa kwa bidii kuelekea pambano hilo, lakini alijikuta akiwa katika hali isiyokuwa nzuri ulingoni, jambo lililoathiri mwenendo wake wa mashambulizi na ulinzi.
Hata hivyo, mashabiki wa ngumi nchini Tanzania na kwingineko wameendelea kutoa maoni tofauti mitandaoni, ambapo wengi wamempa moyo na kumtaka asikate tamaa, wakiamini bado ana nafasi ya kurudi kwa nguvu zaidi.
Kwa upande mwingine, baadhi ya mashabiki wamehoji maandalizi yake na kiwango cha utimamu wake kabla ya pambano hilo, wakisema kuna mambo yanahitaji kufanyiwa kazi kabla ya pambano lijalo.
Pamoja na matokeo hayo, Mwakinyo ameashiria kuwa huu si mwisho wake, bali ni sehemu ya safari ya mchezo wa ngumi unaohitaji uimara, nidhamu na maandalizi ya hali ya juu.