×

Nyumba ya Familia Yauzwa Kisa Fidia ya Shilingi Milioni Moja, Mama Aomba Msaada – Video

Mariamu Gwaruda, mkazi wa Kijiji cha Mwada wilayani Babati mkoani Manyara, ameiomba serikali kuingilia kati mgogoro wa fidia uliodumu tangu mwaka 2022 kati ya familia yake na mzazi wa mtoto aliyedaiwa kugongwa na mume wake kwa pikipiki, mgogoro ambao umesababisha nyumba yao kuuzwa kwa amri ya Mahakama ya Mwanzo ya Mwada na kuwaacha yeye pamoja na watoto wake bila makazi.

Chanzo cha mgogoro huo ni tukio lililotokea mwaka 2022 ambapo mume wa Mariamu, alidaiwa kumgonga mtoto mdogo kwa pikipiki na kusababisha majeraha yaliyohitaji matibabu ambapo mzazi wa mtoto huyo alifungua kesi mahakamani akidai fidia ya gharama za matibabu.

Kwa mujibu wa Mariamu mahakama ilitoa uamuzi wa kulipa fidia ya Shilingi milioni 1.019, jambo ambalo baadaye lilisababisha nyumba yao kuuzwa ili kutekeleza amri hiyo ya mahakama.

Naye Mwenyekiti wa Kitongoji cha Burunge B, Gabriel Pamphil, amesema hajawahi kuona nyaraka zozote za mauzo ya nyumba hiyo wala kupewa taarifa rasmi kuhusu mchakato huo.

Hata hivyo, Mkurugenzi wa Kampuni ya Kibaigwa inayojihusisha na udalali, Jeremiah Mtagwa, amesema taratibu zote za kisheria zilifuatwa katika mchakato wa kuuza nyumba hiyo na kwamba hatua zilizochukuliwa zilikuwa ni utekelezaji wa amri ya mahakama.

Leave a Comment