
Serikali imesema katika mwaka wa fedha 2026/25 imepanga kutoa msamaha wa kodi ya mapato kwa wafanyabiashara wapya kwa kipindi cha mwaka mmoja tangu tarehe ya kupata namba ya utambulisho wa mlipakodi.
Imefafanua kuwa hatua hiyo ni sehemu ya jitihada za Serikali za kuendelea kuweka mazingira wezeshi ya kuvutia urasimishaji wa sekta isiyo rasmi ambayo inaajiri zaidi vijana na wanawake.
Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar ameeleza hayo leo Alhamisi Juni 11,2026 wakati akiwasilisha mapendekezo ya bajeti kuu ya Serikali kwa mwaka 2026/27 bungeni jijini Dodoma, tukio linalofuatilia mubashara na Rais Samia Suluhu Hassan.
“Hatua nyingine ni kufanya maboresho kwenye Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa, Sura 290, ili kuwezesha Mamlaka za Serikali za Mitaa kutenga asilimia 15 ya mapato ya ndani badala ya asilimia 10 ya mikopo ya vijana, wanawake na wenye ulemavu,” ameeleza Balozi Omar.
Balozi Omar amesema kati ya asilimia 15 zitakazotengwa asilimia 10 zitaendelea kuelekezwa kwenye makundi ya wanawake, vijana na wenye ulemavu huku asilimia tano ikitumika kwa ajili ya uwekezaji wa miradi, ujenzi na maboresho ya masoko na maeneo ya ujenzi, biashara na masoko.
“Hii itavutia na kuongeza fursa za ajira kwa vijana, wanawake na makundi maalumu,” amesema Balozi Omar.