×

Coca-Cola Yazindua Kampeni Ya Kombe La Dunia La FIFA 2026 Kuwaunganisha Watanzania Kupitia Soka

Dar es Salaam, Juni 11, 2026 – Kampuni ya Coca-Cola Tanzania imezindua rasmi kampeni ya Kombe la Dunia la FIFA 2026™ inayolenga kuwaunganisha Watanzania kupitia mapenzi yao ya soka, huku ikiwapa fursa ya kushiriki kwa karibu zaidi msisimko, burudani na shamrashamra za michuano hiyo mikubwa zaidi ya soka duniani.

Kampeni hiyo ya kitaifa, iliyoanza tarehe 11 Juni hadi Julai 19, 2026, inatarajiwa kuwafikia maelfu ya mashabiki wa soka nchini kupitia shughuli mbalimbali za burudani, promosheni maalum na matukio ya kutazama mechi kwa pamoja katika maeneo mbalimbali nchini.

Uzinduzi wa kampeni hiyo unaendelea kuonesha dhamira ya Kampuni ya Coca-Cola katika kutumia nguvu ya michezo kuleta watu pamoja, kuimarisha mshikamano wa kijamii na kuifanya Tanzania kuwa sehemu inayofurahia ujio wa Kombe la Dunia 2026.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni hiyo, Mkurugenzi wa Masoko wa Kampuni ya Coca-Cola Tanzania, Bi. Kabula Nshimo, alisema soka lina uwezo wa kipekee wa kuwaunganisha watu kutoka makundi mbalimbali ya kijamii na kuwapa nafasi ya kushiriki hisia na kumbukumbu zinazodumu.

“Kombe la Dunia ni zaidi ya mashindano ya soka. Ni tukio linalowaunganisha watu, familia na marafiki kupitia hisia za pamoja. Kupitia kampeni hii, tunawapa Watanzania fursa ya kushiriki kikamilifu msisimko wa Kombe la Dunia la FIFA 2026™ na kusherehekea kila hatua ya mashindano hayo kama jamii moja,” alisema.

Kwa mujibu wa Coca-Cola, kampeni hiyo itashirikisha zaidi ya maduka 15,000 ya rejareja, migahawa, kumbi za burudani na vituo vya vyakula kote nchini. Ushiriki wa biashara hizo unatarajiwa kuongeza mwamko wa shughuli za kiuchumi katika kipindi cha mashindano huku ukiwapa mashabiki maeneo zaidi ya kukutana na kufuatilia mechi kwa pamoja.

Mbali na kufurahia mechi, watumiaji wa bidhaa za Coca-Cola watapata fursa ya kushinda zawadi mbalimbali na kupata bidhaa maalum zenye nembo ya Kombe la Dunia la FIFA 2026™, zilizotengenezwa mahsusi kwa ajili ya mashindano hayo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Coca-Cola Kwanza Ltd, David Chait, alisema kampeni hiyo imejengwa katika kuenzi hisia zote zinazofanya soka kuwa mchezo unaopendwa na mamilioni ya watu duniani.

“Soka huleta furaha, matumaini, msisimko na wakati mwingine huzuni. Kupitia kampeni hii, tunataka kuwa sehemu ya safari hiyo ya kihisia kwa mashabiki wetu, huku tukiwapa uzoefu unaowafanya wajisikie karibu zaidi na Kombe la Dunia na kuunganishwa na mashabiki wengine kote nchini,” alisema.

Kwa takribani miongo mitano, Coca-Cola imeendelea kuwa mshirika wa FIFA katika kuleta uzoefu wa kipekee wa soka kwa mashabiki duniani. Kupitia kampeni ya mwaka huu, kampuni hiyo inalenga kuhakikisha Watanzania wanakuwa sehemu ya historia ya Kombe la Dunia la FIFA 2026™, mashindano yatakayohusisha timu nyingi zaidi, wachezaji wengi zaidi na mechi nyingi zaidi kuwahi kushuhudiwa katika historia ya michuano hiyo.

Kupitia kampeni hii, Coca-Cola inawaunganisha Watanzania katika kusherehekea mchezo wa soka, huku ikibadilisha nyakati za kawaida kuwa kumbukumbu za pamoja zitakazoifanya safari ya Kombe la Dunia la FIFA 2026™ kuwa ya kipekee kwa mashabiki nchini kote.

Leave a Comment