×

Ivory Coast Yaanza Kombe la Dunia kwa Ushindi wa Kishujaa dhidi ya Ecuador

Timu ya taifa ya Ivory Coast imeanza vyema kampeni yake ya Kombe la Dunia 2026 baada ya kuibuka na ushindi mwembamba wa bao 1-0 dhidi ya Ecuador katika mchezo wa Kundi E uliochezwa jijini Philadelphia.

Shujaa wa mchezo huo alikuwa Amad Diallo ambaye alitokea benchi na kufunga bao la ushindi dakika ya 90, akimalizia kwa ustadi krosi ya Wilfried Singo na kuipa timu yake pointi tatu muhimu.

Ushindi huo umeiwezesha Ivory Coast kupata ushindi wake wa kwanza kabisa dhidi ya timu kutoka Amerika Kusini katika historia ya Kombe la Dunia, huku pia ikiikatisha Ecuador rekodi ya mechi 19 mfululizo bila kupoteza.

Licha ya ushindi huo, nyota kijana mwenye umri wa miaka 19, Yan Diomande, ndiye aliyevutia macho ya wengi kutokana na kiwango chake bora uwanjani. Kiungo huyo aliwasumbua mara kwa mara mabeki wa Ecuador kwa kasi, ubunifu na uwezo wake wa kutengeneza nafasi za mabao.

Ecuador walikuwa na nafasi nzuri za kufunga katika kipindi cha kwanza kupitia John Yeboah na Alan Minda, lakini juhudi zao ziligonga mwamba baada ya mipira yao kugonga mwamba wa lango.

Ivory Coast nao walitengeneza nafasi kadhaa kupitia Nicolas Pepe, Elye Wahi na Singo, lakini walikosa umakini wa kumalizia mashambulizi yao hadi pale Diallo alipoibuka mwishoni mwa mchezo na kuamua matokeo.

Katika kipindi cha pili, Ecuador walijaribu kuongeza kasi ya mashambulizi huku Gonzalo Plata akimlazimisha kipa Yahia Fofana kufanya kazi ya ziada, lakini safu ya ulinzi ya Ivory Coast ilisimama imara.

Bao la Amad Diallo dakika za mwisho liliwafanya mashabiki wa Ivory Coast kushangilia kwa furaha kubwa na kuipa timu hiyo mwanzo mzuri katika kundi ambalo pia linajumuisha Ujerumani na Curaçao.

Matokeo hayo yanaifanya Ivory Coast kufungana pointi na Ujerumani kileleni mwa Kundi E, huku Ecuador wakianza mashindano kwa kupoteza mchezo wao wa kwanza.

Leave a Comment