Watu sita wamepoteza maisha baada ya helikopta mbili kugongana zikiwa angani na kisha kuanguka katika eneo la maegesho ya magari magharibi mwa jiji la Rio de Janeiro nchini Brazil.
Kwa mujibu wa taarifa za Kikosi cha Zimamoto, ajali hiyo ilisababisha moto mkubwa ulioteketeza takribani magari 20 yaliyokuwa yameegeshwa katika eneo hilo, likiwemo eneo la maegesho ya magari ya umeme.
Taarifa za awali zinaeleza kuwa helikopta hizo ziligongana zikiwa safarini kabla ya kupoteza mwelekeo na kuanguka, jambo lililosababisha mlipuko mkubwa na moto uliosambaa kwa haraka.
Mamlaka za Brazil zimethibitisha kuwa watu sita waliokuwa ndani ya helikopta hizo wamefariki dunia, huku taarifa za mwanzo zikionyesha kuwa wote walikuwa wahudumu wa ndege.
Meya wa Rio de Janeiro, Eduardo Cavaliere, amesema baadhi ya watu waliokuwa ndani ya moja ya helikopta hizo walikuwa raia wa kigeni, ingawa hakutoa maelezo zaidi kuhusu mataifa yao.
Polisi pia wameeleza kuwa jina la mwanamuziki wa Marekani, Oliver Tree, limeonekana kwenye orodha ya abiria wa moja ya helikopta hizo. Hata hivyo, bado haijathibitishwa rasmi kama alikuwa miongoni mwa waliofariki kutokana na mchakato wa utambuzi wa miili kuendelea.
Mamlaka husika zimebainisha kuwa utambulisho wa wahanga bado haujakamilika kwa sababu miili yao iliungua vibaya wakati wa ajali hiyo.
Wachunguzi wa usafiri wa anga wameanza uchunguzi wa kina kubaini chanzo cha ajali hiyo, huku shughuli za uokoaji na ukusanyaji wa ushahidi zikiendelea katika eneo la tukio.
Ajali hiyo imeacha simanzi kubwa kwa wakazi wa Rio de Janeiro na kuzua maswali kuhusu usalama wa safari za anga katika eneo hilo.
