
Marius Borg Høiby, mtoto wa miaka 29 wa Malkia wa Norway, Mette-Marit, amehukumiwa kifungo cha miaka minne gerezani baada ya Mahakama ya Wilaya ya Oslo kumpata na hatia ya makosa mawili ya ubakaji.
Uamuzi huo ulitolewa na majaji watatu wa mahakama hiyo, ambao pia walimuondolea mashitaka mengine mawili ya ubakaji, lakini wakamkuta na hatia ya makosa mengine kadhaa aliyokuwa akikabiliwa nayo.
Høiby hakuhudhuria mahakamani wakati hukumu ikisomwa, bali alifuatilia mwenendo wa kesi hiyo kwa njia ya mawasiliano ya video.
Awali, waendesha mashtaka walikuwa wameiomba mahakama imfunge jela kwa miaka saba na miezi saba, huku mawakili wa utetezi wakitaka apewe adhabu isiyozidi miezi 18. Baada ya hukumu hiyo, upande wa utetezi umeonyesha uwezekano wa kukata rufaa.
Marius Borg Høiby si mwanachama rasmi wa familia ya kifalme ya Norway, licha ya kulelewa ndani ya mazingira ya kifalme baada ya mama yake kuolewa na familia hiyo akiwa na umri wa miaka minne.
Hukumu hiyo imekuja wakati ambapo Malkia Mette-Marit anakabiliwa na changamoto kubwa za kiafya, baada ya kuripotiwa kuwa katika hali mbaya na kuorodheshwa miongoni mwa wagonjwa wanaosubiri kupandikizwa mapafu.
Kutokana na hali hiyo, mawakili wa Høiby wamekuwa wakiomba mara kwa mara aachiliwe kwa dhamana au apewe ruhusa maalumu kutoka gerezani ili aweze kutumia muda na mama yake ambaye afya yake inaendelea kudorora.