
Mbunge wa Bunda Mjini, Ester Bulaya amesema Tanzania inaweza kufikia lengo la kujitegemea kiuchumi iwapo kutakuwa na nidhamu ya hali ya juu katika ukusanyaji wa mapato, matumizi ya fedha za umma na uwajibikaji wa watendaji wa Serikali.
Akichangia Mapendekezo ya Bajeti Kuu ya Serikali bungeni jijini Dodoma Juni 16, 2026, Bulaya amesema ni muhimu kupunguza matumizi yasiyo ya lazima serikalini ili kuongeza nafasi ya kuelekeza fedha zaidi kwenye miradi ya maendeleo inayowanufaisha wananchi moja kwa moja.
Ametolea mfano matumizi makubwa ya mafuta kwenye magari ya serikali, akisema kama yakidhibitiwa yanaweza kuokoa fedha nyingi zitakazotumika katika sekta muhimu kama afya, elimu na miundombinu.
Aidha, Bulaya amepongeza uamuzi wa Serikali kuondoa baadhi ya tozo kwa magari yanayotumia gesi na umeme, akisema hatua hiyo itapunguza gharama za uendeshaji na kuchochea uwekezaji katika nishati safi na endelevu.
Pia ameunga mkono hatua ya Serikali kuelekeza zaidi ya asilimia 70 ya fedha za mifuko maalumu moja kwa moja kwenye akaunti husika, akisema itasaidia kuharakisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo kama barabara, maji, nishati vijijini na reli.
Kwa ujumla, amesema nidhamu ya matumizi ya fedha za umma ndiyo msingi muhimu wa kufanikisha maendeleo ya haraka na kujenga uchumi imara wa Taifa.