×

Mbunge Shadya Akemea Mijadala ya Muungano Inayoweza Kuligawa Taifa

Mbunge wa Viti Maalum Kaskazini Unguja kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Shadya Haji Omar, leo Juni 17, 2026, amechangia mjadala wa Bajeti Kuu ya Serikali bungeni jijini Dodoma.

Katika mchango wake, Shadya amekemea vikali vitendo vinavyoendelea kufanyika mitandaoni pamoja na baadhi ya mijadala inayobebwa na wabunge kuhusu suala la Muungano, akieleza kuwa baadhi ya hoja hizo zinaelekea kuligawa taifa.

Amesema ana imani kubwa na Muungano wa Tanzania, akibainisha kuwa kwa sasa Muungano huo si wa kuchanganya mchanga kama ilivyofanywa na waasisi wake, bali umekuwa Muungano wa damu unaounganisha familia na kuimarisha mshikamano wa Watanzania.

Shadya amewataka wabunge pamoja na wananchi kuepuka mijadala inayoweza kuvuruga au kudhoofisha Muungano, akisisitiza kuwa hatua hiyo haina tija kwa taifa na inaweza kuathiri umoja na amani iliyojengwa kwa miaka mingi.

Aidha, ameeleza kuwa ni muhimu kwa viongozi kuendelea kuuenzi na kuulinda Muungano kwa maslahi ya kizazi cha sasa na kijacho.

Leave a Comment