
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Mahusiano), Mhe. Deus Sangu, amepongeza waajiri nchini wanaotekeleza wajibu wao kwa kuzingatia sheria za kazi, ikiwemo kuwasilisha michango ya wafanyakazi katika Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) kwa lengo la kulinda maslahi ya wafanyakazi dhidi ya madhara yanayotokana na kazi.
Mhe. Sangu ametoa pongezi hizo leo Juni 18, 2026, jijini Mwanza wakati wa ziara yake ya kikazi katika viwanda vya Ziwa Steel na Nyanza Bottling Company, ambapo alijionea utekelezaji wa sheria za kazi na ustawi wa wafanyakazi katika maeneo hayo ya uzalishaji.
Amesema kampuni hizo ni mfano mzuri wa kuigwa kutokana na namna wanavyotekeleza wajibu wa kuwasajili wafanyakazi katika mifuko ya hifadhi ya jamii na kuwasilisha michango yao kwa wakati, hatua inayochangia kulinda maslahi ya wafanyakazi na kuimarisha mahusiano bora kazini.
“Serikali imeendelea kusimamia kwa karibu utekelezaji wa sheria za kazi ili kuhakikisha wafanyakazi wanapata haki zao stahiki na wanafanya kazi katika mazingira salama, yenye tija na yanayozingatia utu wa mfanyakazi,” alisema Mhe. Sangu.
Katika hatua nyingine, Waziri Sangu amewahimiza waajiri wote nchini kuhakikisha wanatoa mikataba ya ajira kwa wafanyakazi wao kwa mujibu wa sheria, kuwasajili katika Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), pamoja na kuwasilisha michango kwa wakati ili kulinda maslahi yao ya sasa na ya baadaye.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa waajiri kuzingatia haki zote za msingi za wafanyakazi na kuhakikisha wanalipwa stahiki zao kwa mujibu wa sheria na kanuni zilizowekwa.
Sambamba na hilo, Mhe. Sangu ametoa onyo kwa waajiri wanaokiuka sheria za kazi, akieleza kuwa Serikali haitasita kuchukua hatua za kisheria dhidi ya watakaobainika kukiuka masharti ya ajira, ikiwemo kushindwa kulipa kima cha chini cha mshahara kilichowekwa na Serikali.
“Waajiri wote wanapaswa kuzingatia kima cha chini cha mshahara na sheria zote za kazi. Wale watakaobainika kukiuka masharti hayo watawajibishwa kwa mujibu wa sheria,” alisisitiza.
Ameongeza kuwa afya, usalama na ustawi wa wafanyakazi ni nguzo muhimu katika kuongeza tija, kuimarisha uzalishaji na kuchochea maendeleo ya uchumi wa Taifa. Kutokana na hilo, ameliagiza Shirika la Afya na Usalama Mahali pa Kazi (OSHA) kuendelea kuimarisha ukaguzi katika maeneo ya kazi ili kuhakikisha sheria, kanuni na taratibu za afya na usalama kazini zinazingatiwa kikamilifu.
Naye, Mwanasheria wa Ziwa Steel,Philip Sylivinus, Ziwa Steel, ameishukuru Serikali kwa kuanzisha mifumo ya kidijitali NSSF Portal na WCF Portal, ambayo imerahisisha utoaji wa huduma na kusaidia kutatua changamoto kwa haraka na kwa ufanisi.
Kwa upande wake, Afisa Rasilimali Watu wa Nyanza Bottling, Cecilia Malesa, alisema kampuni hiyo imeendelea kulipa wafanyakazi wake kwa wakati na kuimarisha mazingira bora ya kazi kwa lengo la kuongeza ustawi wa wafanyakazi pamoja na ufanisi wa uzalishaji.
Ziara ya Waziri Sangu jijini Mwanza ni sehemu ya juhudi za Serikali za kufuatilia utekelezaji wa sheria za kazi, kuimarisha mahusiano mema kati ya waajiri na wafanyakazi, na kuhakikisha haki, usalama na ustawi wa wafanyakazi vinaendelea kulindwa katika sekta mbalimbali za uzalishaji
nchini.