×

Waziri Mkuu: Ufugaji Wa Kisasa Ni Jawabu La Migogoro Ya Wakulima Na Wafugaji


WAZIRI Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba amewataka wafugaji nchini kuanzisha mashamba ya malisho na kutumia teknolojia za kisasa za ufugaji ili kuongeza tija na kupata suluhisho la kudumu la migogoro kati ya wakulima na wafugaji inayochangiwa na ongezeko la matumizi ya ardhi.

Akifungua Maonesho ya Tri-Nations Livestock Expo yaliyofanyika Ubena, Wilaya ya Chalinze mkoani Pwani, Ijumaa Juni 19, 2026, Dkt. Mwigulu amesema ongezeko la idadi ya watu na matumizi ya ardhi linaifanya nchi kutafuta mbinu endelevu za kuhakikisha shughuli za ufugaji zinaendelea kwa tija bila kuibua migogoro.

“Hata tusingependa kufanya hivyo, hatuna njia nyingine kwa sababu ongezeko la matumizi ya ardhi linalosababishwa na ongezeko la idadi ya watu, huku ardhi ikiwa haiongezeki, linatulazimu kutafuta suluhisho endelevu,” amesema Dkt. Mwigulu.

Amesema changamoto ya upatikanaji wa malisho inapaswa kwenda sambamba na matumizi ya mbegu bora za mifugo na malisho ili kuwawezesha wafugaji kupata maziwa mengi na nyama nyingi hata kwa kuwa na mifugo michache.

Aidha, Dkt. Mwigulu amewataka wafugaji wa Kitanzania kuyatumia maonesho hayo kama shamba darasa la kujifunza ufugaji bora, wa kisasa na wenye tija ili kuongeza uzalishaji na mchango wa sekta hiyo katika uchumi wa Taifa.

Katika hatua nyingine, Dkt. Mwigulu ametoa wito kwa wadau wa sekta ya mifugo nchini kuchangamkia fursa za matumizi ya teknolojia za kisasa za ufugaji ili kuongeza uzalishaji na kukuza uchumi.

Leave a Comment