
Msanii wa sanaa ya Uigizaji nchini, Jackline Wolper, ameonyesha kumuunga mkono rafiki yake Shamsa Ford kufuatia ujumbe wa huzuni aliouweka hadharani kuhusu changamoto zinazomkabili kwenye ndoa yake.
Kupitia ujumbe wake, Wolper alimpa pole Shamsa na kumtaka awe na moyo wa msamaha na uvumilivu, akisisitiza kuwa anafahamu hali anayopitia na kwamba bado anaamini katika upendo uliopo ndani ya familia hiyo.
“Mamy leo tumeongea karibu masaa mawili, nakuelewa sana. Ila bora wako anakupenda sana na anakuheshimu, please msamehe tu. Mimi nampenda sana Mlilo kwa sababu nakupenda wewe na hao wanangu. Pole, lakini jipe moyo mama, take your time kwanza,” aliandika Wolper.

Kwa upande wake, Shamsa Ford alikanusha madai ya baadhi ya watu waliodai kuwa alichokifanya ni kutafuta umaarufu, akieleza kuwa maumivu ya maisha hayana hadhi wala umaarufu na kila mtu ana njia yake ya kuyaeleza.
“Niko kwenye sanaa zaidi ya miaka 15, mnanijua siku zote mimi si mtu wa drama. Mimi ni mama na nina watoto wawili ambao wako proud na mimi. Hivi naweza kuamua kulia bila sababu yoyote kwenye mtandao?” alihoji Shamsa.
Aidha, Shamsa alisema kuwa kwa sasa anaendelea kupona na kurejea katika hali yake ya kawaida, huku akimshukuru Mungu kwa nguvu anazoendelea kumpa katika kipindi hicho kigumu.
“Namshukuru Mungu, now niko sawa na naendelea kujipona. Mungu pekee ndiye anayejua anapoipeleka hii ndoa. Mungu nipe nguvu tu,” aliandika.