
Stanbic Bank Tanzania imetoa msaada wa Sh milioni 20 kwa Mpango wa Kambi za Matibabu na Upasuaji wa Jumuiya ya Afya ya Afrika Mashariki, Kati na Kusini (ECSA-HC), ili kusaidia upatikanaji wa huduma za afya za kibingwa kwa wananchi katika maeneo yenye uhitaji mkubwa.
Ufadhili huo utasaidia kufanikisha kambi za matibabu na upasuaji bila malipo zitakazofanyika mwezi Julai 2026 katika vituo teule vya afya nchini Malawi pamoja na mikoa ya Arusha na Mtwara nchini Tanzania.
Hundi ya ufadhili ilikabidhiwa na Afisa Mkuu Mtendaji wa Stanbic Bank Tanzania, Bw. Manzi Rwegasira, kwa Mkurugenzi Mkuu wa ECSA-HC, Dkt. Ntuli Angyelile Kapologwe.

Akizungumza katika hafla hiyo, Bw. Rwegasira alisema Benki hiyo inaamini kuwa ushirikiano na wadau mbalimbali ni nguzo muhimu katika kuleta maendeleo endelevu, hususan kupitia uwekezaji katika sekta ya afya.
“Tunatambua kuwa afya bora ni msingi wa maendeleo ya jamii na uchumi. Ufadhili huu unaonesha dhamira yetu ya kuendelea kuwekeza katika ustawi wa wananchi,” alisema.
Kwa upande wake, Dkt. Kapologwe alisema mchango huo utaongeza uwezo wa ECSA-HC kuwafikia wananchi wengi zaidi wanaohitaji huduma za kibingwa, huku akisisitiza umuhimu wa ushirikiano wa sekta binafsi katika kuimarisha mifumo ya afya katika ukanda huo.
Katika kipindi cha mwaka 2025 hadi 2026, Stanbic Bank Tanzania imetoa zaidi ya Sh milioni 230 kwa miradi mbalimbali ya afya na maendeleo ya jamii. Mchango huo unaenda sambamba na maadhimisho ya miaka 30 ya Benki hiyo nchini Tanzania, ikiwa ni sehemu ya juhudi zake za kuendelea kuchangia maendeleo ya kijamii na kiuchumi kupitia sekta za afya, elimu na ustawi wa jamii.
