
TEHRAN, Iran – Mkuu wa mazungumzo wa Iran, Mohammad Bagher Ghalibaf, amesema kuwa Mlango wa Bahari wa Hormuz utasimamiwa na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, kufuatia mazungumzo yaliyofanyika nchini Uswisi yenye lengo la kumaliza vita kati ya Iran, Marekani na Israel.
Akizungumza baada ya kurejea kutoka mazungumzo hayo, Ghalibaf alisema kuwa mlango huo muhimu kwa usafirishaji wa mafuta duniani hautarejea katika hali yake ya kabla ya vita.
“Mlango wa Bahari wa Hormuz hautarudi tena katika hali yake ya kabla ya vita na utasimamiwa na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa mujibu wa sheria za kimataifa,” alinukuliwa akisema na vyombo vya habari vya serikali ya Iran.

Mazungumzo kati ya Iran na Marekani yalifanyika katika eneo la mapumziko la Burgenstock nchini Switzerland, ambapo pande hizo mbili zilikubaliana kuanzisha njia za mawasiliano ili kuhakikisha usalama wa usafiri wa meli katika Mlango wa Hormuz na kupunguza mvutano wa kijeshi katika eneo la Mashariki ya Kati.
Katika video iliyochapishwa kwenye akaunti yake ya Telegram, Ghalibaf alisema safari hiyo ilizaa mafanikio muhimu, ikiwemo masuala ya Hormuz, mgogoro wa Lebanon, msamaha wa mafuta ya Iran pamoja na kuachiliwa kwa fedha za Iran zilizokuwa zimezuiwa nje ya nchi.
Hatua hiyo imekuja baada ya Marekani kutangaza kusitisha kwa muda baadhi ya vikwazo dhidi ya mafuta ya Iran. Makubaliano hayo pia yanatarajiwa kuipa Tehran nafuu ya vikwazo vya kiuchumi pamoja na kurejeshewa sehemu ya mali zake zilizokuwa zimefungiwa.
Mlango wa Bahari wa Hormuz ni mojawapo ya njia muhimu zaidi duniani kwa usafirishaji wa mafuta na gesi. Iran iliufunga mwanzoni mwa vita kabla ya kuufungua tena wiki iliyopita kufuatia makubaliano ya awali na Marekani.
Hata hivyo, Tehran ilitangaza kuufunga tena mwishoni mwa wiki kutokana na mashambulizi ya Israel nchini Lebanon.
Kwa mujibu wa wapatanishi kutoka Qatar na Pakistan, Iran na Marekani sasa zimekubaliana kuanzisha njia maalum ya mawasiliano ili kuepusha ajali au kutokuelewana na kuhakikisha meli za kibiashara zinapita salama katika njia hiyo ya kimkakati.
Licha ya mvutano huo, kampuni zinazofuatilia usafiri wa baharini zimeripoti kuwa shughuli za meli katika Mlango wa Hormuz zimeendelea kwa kasi kubwa zaidi ikilinganishwa na kipindi cha kabla ya makubaliano ya hivi karibuni kati ya Iran na Marekani.