×

Mkuu wa Wilaya ya Nyasa Afungua Mkutano wa Ujirani Mwema kati ya Tanzania na Msumbiji

Mkuu wa Wilaya ya Nyasa, Mhe. Peres Magiri, kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, leo Juni 23, 2026 amefungua Mkutano wa Ujirani Mwema kati ya Tanzania na Msumbiji unaofanyika katika Ukumbi wa Heritage Cottage, Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma.

Mkutano huo wa siku mbili, unaofanyika kuanzia Juni 23 hadi 24, 2026, umewakutanisha viongozi na maafisa kutoka taasisi mbalimbali za usalama za Tanzania na Msumbiji kwa lengo la kujadili masuala ya kiutendaji yanayohusu usalama, makosa ya kuvuka mipaka, pamoja na kuimarisha ushirikiano katika kupambana na uhalifu wa kimataifa.

Akifungua mkutano huo, Mhe. Magiri alisisitiza umuhimu wa kuendeleza ushirikiano wa karibu kati ya mataifa hayo mawili ili kudumisha amani, usalama na utulivu katika maeneo ya mipakani.

Alieleza kuwa mikutano ya aina hiyo imeendelea kuwa jukwaa muhimu la kujenga mahusiano mazuri, kuimarisha mawasiliano na kutafuta suluhisho la pamoja kwa changamoto za kiusalama zinazojitokeza katika maeneo ya mipaka.

Washiriki wa mkutano huo wanatarajiwa kujadili masuala mbalimbali yanayohusu usalama wa wananchi, udhibiti wa uhalifu wa kuvuka mipaka, usimamizi wa mipaka pamoja na njia za kuendeleza ushirikiano wa kiutendaji kati ya vyombo vya usalama vya Tanzania na Msumbiji kwa manufaa ya mataifa yote mawili.

Aidha, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Marco G. Chilya, alipata fursa ya kumtambulisha Kamanda wa Jimbo la Niassa nchini Msumbiji, Kamishna Msaidizi wa Polisi Celestino Albano Vianeque, kabla ya kuanza kwa kikao kazi hicho.

Leave a Comment