Bunge la Seneti la Marekani linalodhibitiwa na chama cha Republican limeidhinisha mswada ambao utamlazimu Rais wa Marekani Donald Trump kusitisha vita na Iran au kutafuta kibali cha bunge kabla ya kuendelea na hatua za kijeshi.
Katika kura iliyopigwa Jumanne jioni, maseneta kadhaa wa chama cha Republican walijiunga na wenzao wa Democratic kupitisha mswada huo kwa kura 50 dhidi ya 48, hatua inayoonyesha upinzani wa pande mbili dhidi ya kuendeleza vita.
Mswada huo pia ulipitishwa katika Bunge la Wawakilishi la Marekani mwezi Juni, ambapo wabunge wanne wa Republican walipiga kura ya ndio pamoja na wabunge wate wa Dempcratic wote, na matokeo yakiwa 215 kwa 208.
Hii ni mara ya kwanza tangu kupitishwa kwa Sheria ya Nguvu za Kivita mwaka 1973 ambapo mabunge yote mawili ya Marekani yamepitisha azimio la pamoja la kusitisha hatua ya kijeshi ya rais.
Hata hivyo, azimio hilo kwa kiasi kikubwa ni la kiishara, kwani licha ya kuidhinishwa na mabunge yote mawili, halitatumwa kwa rais kutiwa saini na halilazimishi kisheria.
Umuhimu wa kura hii ni kwamba inaongeza shinikizo kwa Ikulu ya White House kumaliza vita na Iran, haswa wakati huu ambapo bei ya mafuta imepanda na upinzani wa umma dhidi ya vita hivyo umeongezeka.
Hata hivyo, afisa wa Ikulu ya White House aliambia BBC kwamba tangu makubaliano ya kusitisha mapigano yalikubaliwa Aprili 7, kwa sasa hakuna mzozo wowote ambao utahitaji kuondolewa kwa wanajeshi wa Marekani.