
DUBAI – Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, amesema kuwa taifa hilo linapaswa kuimarisha sekta yake ya ulinzi na kupunguza utegemezi wa silaha kutoka mataifa ya nje, huku akisisitiza umuhimu wa kujenga uwezo wa kujitegemea katika uzalishaji wa vifaa vya kijeshi.
Netanyahu alitoa kauli hiyo Jumanne wakati wa mkutano na maafisa wa akiba wa jeshi katika Kibbutz Migdal Oz, eneo la Gush Etzion, ambapo alizungumzia changamoto mbalimbali za kiusalama zinazolikabili taifa hilo.
Alisema anaithamini sana Marekani kwa msaada ambao imekuwa ikiipatia Israel kwa miaka mingi, lakini sasa ni wakati wa Israel kujenga mfumo wake wa kujitegemea wa uzalishaji wa silaha.
“Ninathamini sana msaada ambao tumepokea kutoka kwa marafiki zetu wa Marekani. Lakini leo nasema wazi kwamba tunahitaji mtandao wetu wa kujitegemea wa silaha. Lazima tutengeneze silaha zetu wenyewe,” alisema Netanyahu.
Kiongozi huyo alieleza kuwa Israel bado inakabiliwa na vitisho kutoka Iran na washirika wake wa kikanda, akidai kuwa ingawa Israel imefanikiwa kutoa pigo kwa maadui wake, mapambano bado hayajafikia mwisho.
“Mahali ambapo tutakuwa miaka 30 ijayo tutategemea nguvu zetu wenyewe,” alisema.
Netanyahu alisisitiza kuwa Israel inapaswa kuongeza uzalishaji wa vifaa vya kijeshi, kuwekeza zaidi katika teknolojia za kisasa za ulinzi na kuandaa kizazi kipya cha makamanda wa jeshi watakaoweza kukabiliana na changamoto za baadaye.
Kauli hiyo imekuja katika kipindi ambacho Mashariki ya Kati inaendelea kushuhudia mvutano mkubwa wa kisiasa na kijeshi, huku Israel ikijaribu kuimarisha uwezo wake wa kujilinda dhidi ya vitisho vinavyojitokeza katika eneo hilo.