×

Tamthilia ya Huba Yaaga Rasmi Baada ya Miaka 10 na Misimu 14 ya Mafanikio

Baada ya kuwaburudisha watazamaji kwa kipindi cha miaka 10, tamthilia maarufu ya Huba itafikia tamati rasmi Julai 6, 2026 kupitia kituo cha Maisha Magic Bongo, ikihitimisha safari yake ya misimu 14 iliyoweka historia katika tasnia ya televisheni Tanzania.

Ilipozinduliwa mwaka 2016, Huba ilikuwa telenovela ya kwanza kurushwa na Maisha Magic Bongo na pia telenovela ya kwanza kuzalishwa nchini Tanzania. Tangu wakati huo, imekuwa moja ya tamthilia zilizofanikiwa zaidi nchini, ikichangia kwa kiasi kikubwa ukuaji wa tasnia ya televisheni, kuibua vipaji vipya na kuthibitisha kuwa hadithi za Kitanzania zinaweza kuvutia watazamaji na wawekezaji.

Mtayarishaji na mkurugenzi wa tamthilia hiyo, Aziz Mohammed, amesema mafanikio makubwa ya Huba ni kubadilisha mtazamo kuhusu uwezo wa tasnia ya filamu na televisheni nchini.

“Huba imeonyesha kuwa Watanzania wanaweza kusimulia hadithi bora na kwamba kuna soko kubwa la kazi hizo,” amesema.

Kwa miaka yote ya uendeshaji wake, Huba imekuwa daraja la mafanikio kwa waigizaji wengi. Mwigizaji Nelly Kamwelu amesema Aziz Mohammed ndiye aliyemfungulia mlango wa kuingia katika tasnia ya uigizaji.

Naye Jacob Steven amesema Huba ilikuwa hatua muhimu katika maisha yake ya kisanii na ilimsaidia kujijengea jina ndani ya tasnia hiyo.

“Maisha Magic Bongo ni moja ya majukwaa yaliyonipa kutambulika zaidi na kunifanya kuwa msanii mwenye kuaminika katika tasnia ya filamu Tanzania,” amesema.

Kwa upande wake, Getrude Mwita amesema safari yake ya miaka tisa ndani ya Huba imemjenga kitaaluma na kumwezesha kushinda tuzo ya Mwigizaji Bora wa Kike mara tatu.

Mwigizaji Kidoa Salum ameeleza jinsi tamthilia hiyo ilivyokuwa sehemu ya maisha yake binafsi, akibainisha kuwa alipata ujauzito akiwa akiigiza Huba na baadaye mtoto wake akaingia pia kuigiza katika tamthilia hiyo.

Kwa upande wa Vincent Kigosi, Huba ilikuwa ndoto ya kila msanii.

“Huba ilikuwa kama Real Madrid; kila nyota ilitamani kucheza humo,” amesema.

Mkongwe wa filamu Tanzania, Riyama Ally, amesema mchango wa Huba katika tasnia hauwezi kusahaulika.

“Huba ilikuwa kama tingatinga; imefungua njia kwa tamthilia nyingi zilizokuja baadaye,” amesema.

Licha ya kufikia mwisho wake, waigizaji na watayarishaji wanaamini kuwa urithi wa Huba utaendelea kuishi kupitia vipaji ilivyokuza, nafasi za ajira ilizozalisha na mchango wake katika kuimarisha tasnia ya burudani nchini Tanzania.

Leave a Comment