
Serikali ya Australia imetangaza kuongeza mara mbili kiwango cha juu cha faini kwa kampuni za mitandao ya kijamii zitakazokiuka sheria ya kiwango cha chini cha umri wa watumiaji, ambapo sasa zinaweza kutozwa hadi dola za Australia milioni 99 (takribani pauni milioni 51.7).
Chini ya sheria hiyo mpya, Kamishna wa Usalama Mtandaoni (eSafety Commissioner) atapewa mamlaka ya kuzitaka kampuni za mitandao ya kijamii kutoa ushahidi wa hatua walizochukua kuhakikisha wanatekeleza marufuku hiyo.
Tangu Desemba 10, 2025, watoto wenye umri chini ya miaka 16 wamezuiwa kutumia majukwaa 10 makubwa ya mitandao ya kijamii nchini Australia. Hata hivyo, imebainika kuwa watoto wengi bado wanafanikiwa kufungua na kutumia programu hizo.
Serikali imeanzisha uchunguzi dhidi ya majukwaa matano yanayotuhumiwa kutotekeleza sheria hiyo ipasavyo, ambayo ni Facebook, Instagram, Snapchat, TikTok na YouTube.
Licha ya sheria hiyo kuanzishwa mwishoni mwa mwaka jana, serikali imekiri kuwa imekuwa vigumu kuhakikisha inatekelezwa kikamilifu.
Ripoti ya Tume ya eSafety imeonyesha kuwa watoto saba kati ya 10 waliokuwa na akaunti za mitandao ya kijamii kabla ya marufuku hiyo bado wana uwezo wa kufikia baadhi ya huduma hizo.
Katika taarifa yake, serikali imesema kuongezwa kwa adhabu na mamlaka ya Kamishna wa eSafety ni sehemu ya juhudi za kuhakikisha kampuni za teknolojia zinawajibika zaidi kulinda watoto.
Waziri Mkuu wa Australia, Anthony Albanese, amesema kampuni kubwa za teknolojia bado hazifanyi vya kutosha kutekeleza sheria hiyo.
“Bado kuna watoto wengi sana wanaotumia mitandao ya kijamii,” amesema Albanese.
Naye Waziri wa Mawasiliano wa Australia, Anika Wells, amesema hajaridhishwa na juhudi za kampuni hizo, akidai nyingi zinafanya kiwango cha chini kabisa kinachohitajika ili kuonekana zinatii sheria.