×

Maajabu ya Mmea wa Rosemary Kiafya Ambayo Wengi Hawayajui

Mmea wa Rosemary, unaojulikana kitaalamu kama Salvia rosmarinus, umetajwa kuwa miongoni mwa mimea inayotumika sana katika lishe na tiba asili kutokana na virutubisho na misombo yake yenye manufaa kwa mwili.

Kwa mujibu wa wataalamu wa lishe na tiba asili, Rosemary ina viambata vinavyofanya kazi kama antioxidants na anti-inflammatory, vinavyosaidia kulinda seli za mwili dhidi ya uharibifu unaosababishwa na chembechembe huru pamoja na kupunguza uvimbe.

Aidha, tafiti mbalimbali zinaonesha kuwa mmea huo unaweza kusaidia kuboresha kumbukumbu, umakini na hali ya hisia (mood). Inasemekana kuwa katika nyakati za kale, baadhi ya wanafunzi wa Ugiriki walivaa mashada ya Rosemary wakati wa mitihani wakiamini uliwasaidia kuongeza uwezo wa kukumbuka.

Rosemary pia imehusishwa na manufaa mengine ya kiafya, ikiwemo kusaidia kudhibiti kiwango cha sukari kwenye damu, kuimarisha afya ya moyo, kusaidia afya ya macho, ngozi na nywele, pamoja na kuboresha mmeng’enyo wa chakula. Baadhi ya tafiti pia zimeonesha kuwa inaweza kusaidia katika juhudi za kudhibiti uzito inapojumuishwa na mtindo bora wa maisha.

Mbali na matumizi yake ya kiafya, Rosemary hutumika kama kiungo cha kuongeza ladha kwenye vyakula mbalimbali kama nyama choma, mikate, supu na mchuzi. Pia inaweza kutumika kutengeneza chai, mafuta ya nywele au barakoa (mask) kwa ajili ya nywele na ngozi.

Hata hivyo, wataalamu wanasisitiza kuwa Rosemary haipaswi kutumika kama mbadala wa matibabu rasmi. Watu wenye magonjwa sugu, wajawazito au wanaotumia dawa za hospitali wanashauriwa kushauriana na mtaalamu wa afya kabla ya kuitumia kwa kiwango kikubwa au kama tiba.

Leave a Comment