
MAREKANI na Iran wamekubaliana kusitisha mashambulizi ya kijeshi dhidi ya kila upande, hatua inayolenga kupunguza mvutano uliokuwa ukitishia usalama wa usafirishaji katika eneo la Ghuba, hususan kwenye Mlango wa Hormuz.
Kwa mujibu wa taarifa za vyombo vya habari, pande hizo mbili pia zinatarajiwa kukutana Jumanne mjini Doha, Qatar, kwa ajili ya mazungumzo yatakayolenga kurejesha usalama wa baharini na kutatua mgogoro wa usafirishaji katika eneo hilo nyeti.
Afisa mmoja wa ngazi ya juu wa Marekani alisema pande hizo zimekubaliana kusitisha shughuli zote za kijeshi kwa sasa, huku akieleza kuwa meli sasa zinaweza kupita kwa uhuru wakati mazungumzo yakiendelea.

Makubaliano hayo yanakuja baada ya mfululizo wa mashambulizi ya kulipizana kati ya pande hizo, hali iliyozua hofu kubwa kuhusu usalama wa mafuta na gesi duniani, kwani karibu asilimia 20 ya nishati ya dunia hupitia kupitia Hormuz.
Hata hivyo, Iran imeeleza mashaka yake kuhusu utekelezaji kamili wa makubaliano hayo, ikisema bado kuna masharti ambayo hayajatekelezwa kikamilifu, ikiwemo masuala ya fedha zilizozuiwa.
Wachambuzi wa masuala ya kimataifa wanasema mazungumzo ya Doha yatakuwa mtihani muhimu kwa pande zote mbili, huku yakitarajiwa kuamua kama usitishaji huu wa mapigano utadumu au la.