×

Mercedes Yashinda Tena, Russell Aongoza Austrian Grand Prix

SPIELBERG, AustriaGeorge Russell ameibuka mshindi wa mbio za Austrian Grand Prix baada ya kuanza kutoka nafasi ya kwanza (pole position), akipunguza pengo la alama dhidi ya mwenzake wa Mercedes-AMG Petronas Formula One Team, Kimi Antonelli, katika msimamo wa ubingwa wa Formula One.

Russell alimaliza mbio hizo mbele ya Max Verstappen wa Red Bull kwa tofauti ya sekunde 1.6, huku Antonelli akimaliza wa tatu baada ya kumkimbiza Verstappen hadi mwisho wa mbio.

Huu ulikuwa ushindi wa pili wa Russell msimu huu baada ya kushinda mbio za ufunguzi nchini Australia, na ushindi wake wa saba katika taaluma yake ya Formula One.

Baada ya matokeo hayo, Antonelli anaongoza msimamo wa madereva akiwa na alama 171, akifuatiwa na Russell mwenye alama 131, huku Lewis Hamilton wa Ferrari akiwa wa tatu na alama 125 baada ya kumaliza nafasi ya tano.

Katika msimamo wa timu, Mercedes inaongoza ikiwa na alama 302 dhidi ya Ferrari yenye alama 204.

Russell alisema alifurahia kurejea juu ya jukwaa la ushindi, licha ya kukumbwa na hitilafu ya mfumo wa maji wa gari lake katika mbio ambazo zilitangazwa kuwa na hatari kubwa ya joto.

“Nimefurahi kurejea kileleni. Mfumo wa maji ulifeli hivyo nina kiu sana, lakini ushindi huu una maana kubwa kwangu,” alisema Russell.

Nafasi ya nne ilichukuliwa na Oscar Piastri wa McLaren, huku Hamilton akimaliza wa tano. Russell sasa ataelekea kwenye mbio za nyumbani za British Grand Prix akiwa na morali kubwa ya kuendelea kupambana katika mbio za ubingwa wa dunia.

Leave a Comment