Rais wa Shirikisho la Soka la Saudi Arabia, Yasser Al Mashal, amejiuzulu kufuatia kutolewa kwa timu ya taifa ya nchi hiyo katika hatua ya makundi ya Kombe la Dunia.
Katika ujumbe wake kwenye mitandao ya kijamii, Al Mashal amesema kutofuzu kwa timu hiyo kwenda hatua inayofuata ya mashindano hayo ni matokeo ambayo hayaendani kwa namna yoyote na matarajio na malengo ya taifa hilo.
“Kutofuzu kwa timu ya taifa kwenda hatua inayofuata ya Kombe la Dunia ni matokeo yasiyoendana na matarajio yetu,” aliandika Al Mashal kwenye mitandao ya kijamii.
“Ninabeba jukumu kamili kwa matokeo haya na naomba radhi kwa wote waliotarajia kuiona timu yetu ikifanya vizuri zaidi.

Kwa kuamini kwamba uwajibikaji unahitaji kutoa nafasi kwa mwanzo mpya, nimeamua kutoendelea hadi mwisho wa muhula wangu wa uongozi.”
Saudi Arabia ilimaliza mkiani mwa Kundi H ikiwa na pointi mbili, baada ya kutoka sare dhidi ya Uruguay na Cape Verde na kupoteza mechi dhidi ya Hispania.
Al Mashal alikuwa ameongoza Shirikisho la Soka la Saudi Arabia kwa miaka saba na alihusika kwa kiasi kikubwa katika jitihada zilizoiwezesha Saudi Arabia kupata haki ya kuwa mwenyeji wa Kombe la Dunia la mwaka 2034.
Saudi Arabia ilikuwa ikishiriki Kombe la Dunia kwa mara ya tatu mfululizo na mara ya saba kwa ujumla. Hata hivyo, maandalizi yake yaliathiriwa na uamuzi wa kumwondoa kocha Herve Renard na kumteua Georgios Donis chini ya miezi miwili kabla ya mashindano kuanza.