×

Rais Samia Apokea Gawio la Trilioni 1.327, Apongeza Ongezeko la Asilimia 30 (Picha +Video)

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan akihutubia viongozi na wageni mbalimbali baada ya kupokea Gawio na Michango kutoka kwa Taasisi na Mashirika ya Umma, kwenye hafla iliyofanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam, tarehe 30 Juni, 2026.

Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameyataka mashirika na taasisi za umma kuweka mikakati madhubuti ya kujiendesha kwa ufanisi na kupunguza utegemezi wa ruzuku kutoka Serikalini, ili yaweze kuongeza mchango wake katika ukuaji wa uchumi wa taifa.

Rais Samia ametoa agizo hilo leo, Juni 30, 2026, wakati wa hafla ya kupokea gawio na michango kutoka mashirika ya umma iliyofanyika Ikulu, Dar es Salaam.

Rais Samia akitoa Tuzo kwa Taasisi na Mashirika yaliyofanya vizuri katika Makundi mbalimbali ya uchangiaji kwa mwaka 2026, kwenye hafla iliyofanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam, tarehe 30 Juni, 2026.

Amesema ni muhimu kwa mashirika ambayo bado hayajaanza kutoa gawio kwa Serikali kujitathmini na kujifunza kutoka kwa yale yanayofanya vizuri, ili yaweze kuimarisha utendaji wake na kuchangia zaidi mapato ya Serikali.

Rais Samia akipokea Gawio na Michango kutoka kwa Viongozi wa Taasisi na Mashirika ya Umma, kwenye hafla iliyofanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam, tarehe 30 Juni, 2026.

Katika hafla hiyo, Rais Samia amepokea jumla ya shilingi trilioni 1.327 kama gawio na michango kutoka mashirika ya umma yaliyo chini ya usimamizi wa Ofisi ya Msajili wa Hazina (OMH) pamoja na kampuni ambazo Serikali ina hisa chache.

Kiasi hicho ni ongezeko la asilimia 30 ikilinganishwa na mwaka 2025, ambapo Serikali ilipokea shilingi trilioni 1.028.

Akitoa taarifa kuhusu makusanyo hayo, Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu, amesema mashirika na kampuni za kibiashara zimechangia shilingi bilioni 800, sawa na asilimia 60 ya makusanyo yote.

Aidha, amesema michango ya mapato ghafi kutoka taasisi imefikia shilingi bilioni 406, sawa na asilimia 30 ya makusanyo yote, huku mapato mengine yakichangia shilingi bilioni 121, sawa na asilimia 10 ya jumla ya fedha zilizokusanywa.

Mchechu amesema ongezeko hilo limetokana na kuimarika kwa mazingira ya biashara pamoja na utekelezaji wa mageuzi mbalimbali ya kiutendaji, kiusimamizi na kiutawala katika mashirika ya umma, hatua ambazo zimeongeza ufanisi na faida za taasisi hizo.

 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan akipokea Tuzo ya Heshima kutoka kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo pamoja na Msajili wa Hazina Bw. Nehemiah Mchechu kwenye hafla ya kupokea Gawio na Michango ya Taasisi na Mashirika ya Umma, Ikulu Jijini Dar es Salaam, tarehe 30 Juni, 2026.

Leave a Comment