
Bayern Munich imekamilisha usajili wa kiungo mshambuliaji wa Morocco, Ismael Saibari, akitokea PSV Eindhoven kwa ada inayoripotiwa kufikia dola milioni 63 sawa na Shilingi za Tanzania bilioni 163.8.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 25 amesaini mkataba wa muda mrefu utakaomuweka Bayern hadi Juni 2031, na atavaa jezi namba 34 katika klabu hiyo ya Bundesliga.
Bayern imethibitisha kuwa namba hiyo ina maana ya kipekee kwa Saibari, ambaye ameichagua kama heshima kwa rafiki yake Abdelhak Nouri, aliyepata ajali ya kiafya uwanjani mwaka 2017 na kuathiri uwezo wake wa kucheza soka.
Saibari amesema uamuzi huo ni njia ya kumuenzi na kumuunga mkono rafiki yake wa karibu, akibeba ujumbe wa matumaini kupitia jezi hiyo anayovaa.

Nyota huyo wa Morocco amekuwa katika kiwango bora kwenye Kombe la Dunia 2026, akiwa amefunga mabao matatu katika mechi nne na kusaidia taifa lake kufika hatua ya 16 bora.
Pia alitoa mchango muhimu katika ushindi dhidi ya Uholanzi, akifunga penalti ya ushindi iliyoiwezesha Morocco kusonga mbele kwenye michuano hiyo.
Saibari alikuwa miongoni mwa wachezaji muhimu wa PSV Eindhoven, akiisaidia kutwaa ubingwa wa ligi ya Uholanzi mara tatu mfululizo na kutwaa tuzo ya mchezaji bora wa msimu uliopita.