
Wapenzi wawili wamezua mjadala mkubwa nchini Marekani baada ya kupanda hadi kileleni mwa jengo maarufu la Empire State Building lililopo jijini New York na kufanya tukio la uchumba wakiwa juu ya mnara wenye urefu wa futi 1,454, kabla ya kukamatwa na polisi.
Wawili hao, wanaodhaniwa kuwa ni Angela Nikolau na Ivan Beerkus, waliinua bendera yenye ujumbe wa amani uliosomeka, “Nguvu ya upendo inaposhinda tamaa ya madaraka, dunia hupata amani” (When the power of love beats the love of power, the world knows peace), kabla ya Ivan kupiga goti na kumvisha Angela pete ya uchumba.

Baada ya tukio hilo la kimahaba, maafisa wa Polisi wa Jiji la New York (NYPD) walipanda juu ya mnara huo na kuwakamata wawili hao. Video zilizorekodiwa na kamera za maafisa hao (bodycam) zimeonyesha jinsi walivyowashusha kutoka juu ya jengo hilo na kuwaweka chini ya ulinzi.
Angela na Ivan ni maarufu duniani kwa kupanda majengo marefu bila kutumia vifaa vya usalama. Umaarufu wao uliongezeka kupitia filamu ya Netflix Skywalkers: A Love Story, inayosimulia maisha yao na safari za kupanda majengo marefu katika nchi mbalimbali.

Hadi sasa, haijafahamika waliwezaje kufika kwenye sehemu ya juu ya mnara wa Empire State Building, ambao kwa kawaida hulindwa kwa ulinzi mkali.
Tukio hilo liliwashangaza wakazi na watalii waliokuwa eneo hilo, huku wengi wakisimama kutazama operesheni ya polisi iliyohusisha helikopta na vikosi vya uokoaji, kabla ya wawili hao kushushwa salama na kutiwa mbaroni.





