×

Polisi: Ushirikiano na Makampuni ya Ulinzi Ni Silaha Dhidi ya Uhalifu

Jeshi la Polisi limetoa wito wa kuimarishwa kwa ushirikiano kati yake na makampuni binafsi ya ulinzi ili kuongeza ufanisi katika kupambana na uhalifu na kuendelea kudumisha amani na usalama nchini.

Wito huo umetolewa na Naibu Kamishna wa Jeshi la Polisi (DCP), Ulrich Matei, wakati wa hafla iliyoandaliwa na kampuni ya SGA Tanzania kwa ajili ya kuwaaga watumishi waliostaafu na kuwatambua wafanyakazi waliohudumu kwa zaidi ya miaka 20 kupitia programu ya Club 20.

Hafla hiyo ilifanyika katika Bustani ya Hekima jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na viongozi kutoka Jeshi la Polisi, Trade Union Congress of Tanzania (TUCTA), uongozi wa SGA Tanzania, wafanyakazi pamoja na wageni mbalimbali waalikwa.

Akizungumza katika hafla hiyo, DCP Matei alisema sekta binafsi ya ulinzi ina mchango mkubwa katika kuhakikisha usalama wa wananchi na mali zao, hivyo ushirikiano wake na Jeshi la Polisi unapaswa kuendelea kuimarishwa.

Aliwataka watumishi waliostaafu kuendelea kutumia uzoefu wao kuhamasisha amani na usalama katika jamii hata baada ya kumaliza utumishi wao.

DCP Matei pia aliipongeza SGA Tanzania kwa kuendelea kuthamini mchango wa wafanyakazi wake kupitia programu za kuwapongeza waliodumu kazini kwa muda mrefu pamoja na kuwekeza katika ustawi na maendeleo ya watumishi wake.

Alisema makampuni mengi ya ulinzi bado hayajazingatia kikamilifu maelekezo ya kuboresha mazingira ya kazi kwa kutoa mafunzo ya mara kwa mara, kuboresha mishahara, kufanya uhakiki wa watumishi na kuimarisha usimamizi wa kazi.

“SGA mmeonyesha mfano mzuri kwa kutekeleza maelekezo haya. Ni kampuni inayostahili kuigwa na makampuni mengine ya ulinzi binafsi nchini,” alisema.

Aidha, alieleza kuwa hatua ya kampuni hiyo kuwapongeza wafanyakazi zaidi ya 95 waliotumikia kampuni kwa zaidi ya miaka 20 ni ishara ya kuthamini uaminifu na kujituma kazini.

DCP Matei aliwataka wamiliki wa makampuni binafsi ya ulinzi kuendelea kuwekeza katika matumizi ya teknolojia za kisasa, kutoa mafunzo kwa watumishi, kuzingatia sheria pamoja na kuheshimu haki za binadamu ili kuongeza ubora wa huduma na kupunguza malalamiko kutoka kwa wananchi.

Alisisitiza kuwa Jeshi la Polisi litaendelea kushirikiana kwa karibu na makampuni hayo kama sehemu ya juhudi za pamoja za kuimarisha usalama nchini.

Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Fedha wa SGA Tanzania, Jonathan Geleta, aliushukuru uongozi wa Jeshi la Polisi kwa ushirikiano unaoendelea kutolewa kwa makampuni binafsi ya ulinzi.

Aliahidi kuwa SGA itaendelea kufuata sheria, kanuni na miongozo inayotolewa na Jeshi la Polisi ili kuhakikisha huduma zake zinaendelea kuwa za viwango vya juu.

Geleta pia aliwapongeza watumishi waliostaafu kwa mchango wao mkubwa katika mafanikio ya kampuni na kuwataka kuwa mabalozi wa amani na usalama wanaporejea kuishi katika jamii.

SGA Security ni miongoni mwa kampuni kongwe za ulinzi binafsi nchini, ikiwa imeanza shughuli zake zaidi ya miaka 42 iliyopita. Kwa sasa kampuni hiyo inaajiri zaidi ya Watanzania 5,000 na hutoa huduma mbalimbali za ulinzi, usafirishaji wa bidhaa zenye thamani, huduma za dharura pamoja na mifumo ya usalama wa kielektroniki.

Leave a Comment