
Chama cha Gofu cha Wanawake Tanzania (TLGU) kimezindua rasmi Mpango Mkakati wa Miaka Mitano (2026–2030) wenye lengo la kuleta mageuzi katika mchezo wa gofu kwa wanawake na wasichana nchini kupitia ongezeko la ushiriki, ukuzaji wa vipaji na kuinua viwango vya ushindani wa kimataifa.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, Rais wa TLGU, Bi. Timea Chogo, alisema mpango huo unaenda sambamba na dira ya chama ya kuiwezesha Tanzania kuwa miongoni mwa mataifa yanayoongoza barani Afrika katika mchezo wa gofu ya wanawake.
Katika hatua nyingine, Bi. Chogo ametangaza kuwa mashindano ya The Lady President’s Golf Cup 2026 yatazinduliwa rasmi na kufanyika Julai 11, 2026, katika Viwanja vya Gofu vya Lugalo, Dar es Salaam.
Alisema mashindano hayo yatafanyika chini ya kaulimbiu ya “Drive It. Tee the Future”, inayolenga kuhamasisha wanawake na wasichana kujitokeza kushiriki mchezo wa gofu pamoja na kuweka msingi imara wa maendeleo endelevu ya mchezo huo nchini.

Kwa mujibu wa TLGU, mkakati wa miaka mitano unakusudia kujenga mfumo endelevu wa kukuza vipaji vya wanawake na wasichana, kuongeza idadi ya wanawake wanaoshiriki mashindano ya ndani na kimataifa, pamoja na kuhamasisha ushiriki wao katika nafasi za uongozi ndani ya mchezo wa gofu.
Aidha, chama hicho kimeeleza kuwa utekelezaji wa mkakati huo utasaidia kufungua fursa kwa wanawake kufikia ngazi za juu za ushindani, kuwakilisha Tanzania katika mashindano ya kimataifa na kushika nafasi mbalimbali za uongozi ndani na nje ya mchezo wa gofu.
TLGU inaamini kuwa kupitia mpango huo, mchezo wa gofu ya wanawake utaendelea kukua na kuiweka Tanzania katika nafasi nzuri zaidi kwenye ramani ya gofu barani Afrika.
