
Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) limewataka wananchi kupuuza wito wowote unaohamasisha vurugu na uvunjifu wa amani, likisisitiza kuwa hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya mtu yeyote atakayebainika kushiriki katika vitendo vinavyohatarisha usalama wa nchi.
Katika taarifa yake kwa umma, JWTZ limesema lina wajibu wa kulinda usalama wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na wananchi wake kwa mujibu wa Katiba ya mwaka 1977 pamoja na Sheria ya Ulinzi wa Taifa, Sura ya 192.
Jeshi hilo limeeleza kuwa litaendelea kushirikiana na vyombo vingine vya dola kuhakikisha matukio ya vurugu, ghasia na uvunjifu wa amani yanazuiwa na kudhibitiwa kwa mujibu wa sheria.
Aidha, wananchi wamehimizwa kuendelea kushirikiana na mamlaka kwa kutoa taarifa kwa viongozi wa vijiji, mitaa pamoja na vyombo vya ulinzi na usalama kuhusu viashiria vyovyote vya uchochezi au vitendo vinavyoweza kuhatarisha amani na utulivu wa nchi.
JWTZ pia limewahakikishia wananchi kuwa litaendelea kutekeleza majukumu yake ya msingi ya kulinda mipaka ya taifa, Katiba na mamlaka ya nchi, huku likiendelea kushirikiana na wananchi katika kudumisha amani, umoja na maendeleo ya Tanzania.