
Washington, D.C., Marekani – Rais wa Marekani Donald Trump amesema Marekani inaingia katika kile alichokiita enzi ya dhahabu huku akisisitiza kuwa taifa hilo linaendelea kushinda na lina uwezo wa kufikia mafanikio makubwa zaidi.
Akizungumza katika sherehe za kuadhimisha miaka 250 usiku wa kuamkia leo Julai 5, 2026 tangu kuanzishwa kwa Marekani, Trump alisema taifa hilo lina historia ya mafanikio yasiyo na kifani na bado “linaanza safari yake”, akiahidi kulipeleka kwenye viwango vipya vya maendeleo.
Hotuba hiyo ilichelewa kuanza kwa zaidi ya saa mbili kutokana na mvua kubwa, radi na hali mbaya ya hewa iliyotokana na wimbi la joto kali lililokumba maeneo ya mashariki mwa Marekani. Licha ya changamoto hizo, maelfu ya wananchi walirejea kushiriki hafla hiyo iliyohitimishwa kwa fataki kubwa zilizopambwa kama sehemu ya maadhimisho ya kihistoria.

Katika hotuba yake, Trump alisisitiza kuwa “Marekani ni taifa la washindi” na kudai kuwa nchi hiyo imeanza kushinda tena chini ya uongozi wake. Pia aliendelea kukosoa kile alichokiita tishio la ukomunisti nchini humo, akisema mfumo huo hautaruhusiwa kupata nafasi nchini Marekani.
Sherehe hizo pia zilihudhuriwa na maveterani wa jeshi pamoja na wafanyakazi wa misheni ya anga ya Artemis II, huku Trump akitumia fursa hiyo kuzungumzia historia ya Marekani na mchango wake duniani.
Hata hivyo, maadhimisho hayo yaligubikwa na changamoto mbalimbali, ikiwemo kufutwa kwa gwaride la Siku ya Uhuru mjini Washington kutokana na joto kali, pamoja na hatua kali za kiusalama zilizowekwa kuzunguka eneo la Washington Monument. Huduma za dharura ziliripoti kuwahudumia watu zaidi ya 50 waliopata athari zinazohusiana na joto, huku baadhi yao wakipelekwa hospitalini kwa matibabu.
Aidha, viongozi wa upinzani na baadhi ya wachambuzi wamekosoa matumizi ya maadhimisho hayo wakidai yaligeuzwa kuwa jukwaa la kisiasa badala ya tukio la kuwaunganisha Wamarekani wote.