×

Madarasa Mapya, Matumaini Mapya: Uwekezaji Ulivyobadili Mazingira ya Kujifunzia Shule ya Msingi Orng’adida

Babati, Manyara – Kwa miaka kadhaa, wanafunzi wa Shule ya Msingi Orng’adida iliyopo katika Kata ya Quash, Wilaya ya Babati mkoani Manyara, walilazimika kusoma katika mazingira yenye upungufu mkubwa wa madarasa na vyoo, hali iliyoathiri mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji.

Shule hiyo yenye wanafunzi 1,008 ilikuwa na vyumba 11 pekee vya madarasa, idadi ambayo haikukidhi mahitaji ya wanafunzi waliokuwepo. Kutokana na hali hiyo, baadhi ya wanafunzi walilazimika kubanana katika darasa moja, huku wengine wakisoma kwa mfumo wa zamu, ambapo kundi moja lilihudhuria masomo asubuhi na jingine mchana.

Kwa mfano, darasa la tano lilikuwa na wanafunzi 119 katika chumba kimoja cha darasa, huku darasa la saba likiwa na wanafunzi 130 katika darasa moja. Aidha, wanafunzi wa madarasa ya awali, la kwanza na la pili walikuwa wakisoma kwa zamu kutokana na uhaba wa vyumba vya madarasa.

Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Mwajuma Gallas, anasema changamoto hizo zilikuwa zikiathiri ubora wa ufundishaji na ujifunzaji, huku msongamano mkubwa wa wanafunzi ukipunguza ufanisi wa walimu kufundisha.

Kwa upande wake, mwanafunzi wa shule hiyo, Raymond Sulle, anasema mazingira hayo yalikuwa yakifanya ujifunzaji kuwa mgumu kutokana na idadi kubwa ya wanafunzi waliokuwa wakitumia darasa moja.

Mbali na upungufu wa madarasa, shule hiyo pia ilikuwa ikikabiliwa na changamoto ya miundombinu ya vyoo.

Zaidi ya wanafunzi 1,000 walikuwa wakitumia matundu 25 pekee ya vyoo wakati mahitaji halisi ni matundu 45, hivyo kuwepo kwa upungufu wa matundu 20.

Vyoo hivyo vilikuwa vimechakaa na havikukidhi mahitaji ya wanafunzi, hali iliyosababisha msongamano mkubwa na kuongeza hatari ya magonjwa yanayotokana na mazingira yasiyo salama.

Walimu wa shule hiyo, akiwemo Vailet Kwavava, pamoja na Mwalimu Mkuu Mwajuma Gallas, wanasema hata vyoo vya walimu vilikuwa katika hali mbaya, jambo lililoathiri mazingira yao ya kazi.

Hata hivyo, hali hiyo sasa inaanza kubadilika.

Kupitia ushirikiano kati ya Shirika la So They Can na Ubalozi wa Japan nchini Tanzania, shule hiyo imejengewa vyumba vitatu vipya vya madarasa, vyoo vya kisasa vya wavulana na wasichana, choo maalumu kwa wanafunzi wenye ulemavu, sehemu za kunawia mikono pamoja na vyoo vya walimu.

Mkurugenzi wa Shirika la So They Can, Roselyne Mariki, amesema mradi huo uliogharimu zaidi ya shilingi milioni 266 unalenga kuboresha mazingira ya kujifunzia na kuhakikisha watoto wanapata elimu katika mazingira salama na rafiki.

Naye Balozi wa Japan nchini Tanzania, Jin Hashimoto, amesema Japan itaendelea kushirikiana na Tanzania katika kusaidia miradi inayoboresha sekta ya elimu na kuinua ustawi wa watoto.

Walimu na wanafunzi wanaamini kuwa miundombinu hiyo mipya itapunguza msongamano madarasani, kuboresha mazingira ya kujifunzia na kuongeza ari ya wanafunzi kufanya vizuri katika masomo yao.

Nao wazazi wamepongeza utekelezaji wa mradi huo wakisema utachangia kuongeza ubora wa elimu na kuwajengea watoto mazingira salama ya kujifunza.

Akizungumza wakati wa kukabidhi mradi huo, Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mbunge wa Babati Vijijini, Daniel Sillo, amepongeza Serikali ya Japan pamoja na Shirika la So They Can kwa mchango wao katika kuboresha sekta ya elimu nchini.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Babati, Anna Mbogo, amesema Serikali itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha miundombinu ya elimu inaendelea kuboreshwa ili kukidhi mahitaji ya wanafunzi.

Licha ya mafanikio hayo, Shule ya Msingi Orng’adida bado inahitaji madarasa zaidi, ukarabati wa baadhi ya majengo yaliyopo pamoja na jengo la utawala, kwani kwa sasa walimu bado wanalazimika kutumia moja ya vyumba vya madarasa kama ofisi.

Kwa uongozi wa shule, maboresho yaliyofanyika ni mwanzo wa safari ya kufikia mazingira bora ya elimu. Matumaini yao ni kuona mahitaji yaliyosalia yakipatiwa ufumbuzi ili kila mwanafunzi apate fursa ya kujifunza katika mazingira salama, bora na yanayochochea mafanikio ya kitaaluma.

Leave a Comment