
Misri imeibua malalamiko makubwa dhidi ya mwamuzi wa Ufaransa, Francois Letexier, baada ya kufungwa mabao 3-2 na Argentina katika hatua ya 16 bora ya Kombe la Dunia 2026, huku wengi wakidai maamuzi yake yaliinyima timu hiyo ushindi wa kihistoria.
Pharaohs walikuwa mbele kwa mabao 2-0 na walikuwa wamebakiza dakika chache kuiondoa mabingwa watetezi wa dunia, lakini Argentina ilifanya comeback ya kuvutia na kutinga robo fainali.
Malalamiko makubwa yalitokana na mwamuzi kufuta bao la pili la Misri kutokana na faulo iliyodaiwa kutokea awali, pamoja na kukataa kuipa Misri penalti baada ya Mohamed Salah kuchezewa faulo ndani ya eneo la hatari.
Dakika chache baadaye, Argentina ilianzisha mashambulizi ya kushtukiza na kufunga bao la ushindi kupitia Enzo Fernandez.
Hasira ziliendelea kwa benchi la ufundi la Misri, ambapo kocha Hossam Hassan, Hamdi Fathy na kipa Mostafa Shobeir walionywa kwa kadi za njano, huku msaidizi wa kocha Mohamed Abdel Wahed akioneshwa kadi nyekundu.
Misri ilianza mchezo kwa kasi na kupata bao la kwanza kupitia Yasser Ibrahim, aliyefunga kwa kichwa baada ya krosi ya Marwan Attia.
Baadaye, Lionel Messi alipata nafasi ya kusawazisha kwa mkwaju wa penalti, lakini kipa Mostafa Shobeir aliokoa kwa ustadi mkubwa.
Kipindi cha pili, Misri ilionekana kuongeza matumaini baada ya Zico kufunga bao lililowafanya waongoze 2-0, licha ya bao lingine kufutwa mapema kutokana na faulo iliyotafsiriwa na VAR.
Argentina ilianza kurejea mchezoni kupitia Cristian Romero, kabla ya nahodha Lionel Messi kufunga bao la kusawazisha dakika ya 83.
Katika dakika za majeruhi, baada ya Misri kudai kunyimwa penalti kufuatia Salah kuangushwa, Argentina ilifanya shambulizi la haraka na Enzo Fernandez kufunga bao la ushindi lililoivusha timu hiyo kwa ushindi wa mabao 3-2.
Baada ya mchezo huo, mashabiki wengi wa Misri na Waarabu walielezea hasira zao mitandaoni, wakidai kuwa maamuzi ya mwamuzi yaliathiri matokeo ya mechi na kuinyima Misri nafasi ya kuandika historia kwa kuwaondoa mabingwa watetezi wa Kombe la Dunia.